Afisa Utekelezaji Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini katika Kitengo cha Magari Bandari ya Dar es Salaam, Principal Operation Officer and Head of Motor Vehicle Section Dar es Salaam Port), Bw. Daniel Sira (wapili kusho) akiwaonyesha stika kwenye moja ya gari ambalo limekidhi vigezo vyote vya kuondoka bandarini.
Wengine wanaoshuhudia ni Kaimu Meneja wa Mawasiliano wa mamlaka hiyo, Bi. Janeth Ruzangi (katikati), kaimu afisa mawasiliano mkuu, Bw. Peter millanzi (kushoto) na afisa mawasiliano Mwandamizi, Bi. Levina Msia (Kulia). Waandishi wa habari walitembelea kitengo hicho cha kujionea shughuli za upakuaji magari.
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imesema baada maboresho ya vitendea kazi yaliyofanyika bandari hapo hivi karibuni, kitengo cha magari (Motor Vehicle section) kinauwezo wa kupakua magari 1,000 kwa shifti moja ya masaa nane tofauti na kipindi cha nyuma ilikuwa inapakua chini ya magari 400.
Afisa Utekelezaji Mkuu ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Magari Bandari ya Dar es Salaam (Principal Operation Officer and Head of Motor Vehicle Section Dar es Salaam Port),Bw. Daniel Sira aliwaambia waandishi wa habari waliotembelea kujionea upakuaji wa magari bandarini hapo jana kuwa huduma ya upakuaji magari ni nzuri na inafanyika kwa haraka.
“Tumefanya hivi kwa nia ya kutaka kutoa huduma nzuri na kwa haraka kwa wateja wetu wanaoagiza magari na wenye meli wasiweze kutumia muda mwingi katika bandari yetu,” na kuongeza kusema kuwa vifaa na ari ya kufanya kazi kwa bidii ndiyo imeongeza ufanisi huo.
Alisema wameboresha upakuaji kwa kuwa na vifaa vya kutosha katika upakuaji ili kuruhusu meli kukaa muda mfupi bandarini sababu meli ikikaa bandari muda mrefu ni ghrama na hii inavutia wenye meli kuzidi kuleta meli zaidi kwenye bandari hii.
Alifafanua kuwa wamefanya hivyo sababu mwenye meli na wenye magari wote ni wateja wa bandari hivyo wanategemea kazi ifanyike kwa haraka ili waweze kuondoka kwa haraka ndiyo maana wamefanya hivyo kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya wateja wote hao.
Bw.Sira alisema utaratibu wa sasa wa kukaguwa magari wakati wa upakuaji kutoka kwenye meli wafanyakazi wanafanya kwa umakini mkubwa na huweka alama ya stika ya njano kwa magari yasiyo na matatizo ya upungufu wa vyifaa,na alama nyekundu kwa magari yaliyo na vifaa pungufu.
Alisema katika eneo la upakuaji, magari yaliyokamilika vifaa vyote yanaruhusiwa kuondoka katika eneo hilo yakiwa na alama ya stika ya kijani na alama nyekundu kwa yale yenye matatizo kivifaa tangu yakiwa kwenye meli.Shughuli ya ukaguzi huo inafanyika wakati wa upakuaji kutoka kwenye meli ili kuwa na uhakika wa uzima wa magari pindi tu yanapokuwa yanapakuliwa huku wenye meli wakiwa pale kwa ajili ya kukabidhiana.
“Zamani wakati wa upakuaji kulikuwa na ucheleweshaji sababu kila gari likiwa nzima au linamatatizo yote yaliandikiwa formu ya Vehicle Discharge Inspection and Transfer Tally (VDITT) lakini kwa sasa haifanyiki hivyo.
Alisema magari mazima kwa sasa hayaandikiwi fomu hizo, bali yanaruhusiwa kuondoka toka eneo la upakuaji kwa kuwekewa alama ya kijani, na zile zenye matatizo kutoka kwenye meli zinaandikiwa fomu hiyo katika eneo la upakuaji wakati wa makabidhiano na wenye meli ili mamlaka isiweze kuingia garama ambayo haikuhusika.
Alisema pia magari yaliyoshuka ambayo ni mazima lakini yakanyofolewa vifaa bandarini wakati wa makabidhiano na wakala wa mizigo yanaandikiwa fomu ya Vehicle Handover (VHF) ili kuonyesha uharibifu huo umetokea bandarini hapo.
Alisisitiza magari yakiwa na matatizo tangia kwenye meli, wenye meli anakuwa na jukumu la kulipa gharama ya magari kwa wenye magari sababu amesabisha uharibifu huo, na kuongeza kusema kuwa inapotokea magari yamepakuwaliwa yakiwa yamekamilika kivifaa lakini likatokea tatizo la kunyofolewa vifaa yakiwa bandari basi mamlaka inakuwa na jukumu la kulipa gharama hizo kwa wenye magari.
Alisema gari likiwa na stika nyekundu kabla ya mteja kukabidhiwa linakaguliwa upywa kati ya karani wa bandari na wakala wa mzigo, wanasainishana kwa kuangalia vifaa vilichopungua baada ya kushushwa kwenye meli.
“Katika mazingira hayo kama gari limepungua vifaa likiwa kwenye meli mteja anatakiwa kumdai mwenye meli au alikonunua na kama limepungua vifaa likiwa bandarini basi mteja aidai bandari,”.
Pia alitoa wito kwa waagizaji wa magari wauzaji au mtu mmoja mmoja anayeagiza gari kuwa wanatakiwa kudai fomu ya VDITT na VHF ambazo ni nyaraka zinazosaidia kujiridhisha magari yao kama yako salama au vinginevyo.
Alisema wenye magari wanatakiwa kudai fomu hizo kutoka kwa wakala wa mizigo (Clearing and Forwarding Agency) ambao wanakuwa na fomu hizo baada ya makabidhiano kati yao na bandari