POLISI mkoani Mwanza imesema iko tayari kuwadhibiti wahalifu watakaojihusisha na vitendo vya uporaji wa mali za wakazi wa jiji la Mwanza wakati wa sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mwanza, Eliasi Mangu aliyasema hayo jana jijini Mwanza alipokuwa anaelezea mikakati ya jeshi hilo katika kupambana na uhalifu wakati wa maadhimisho ya sikuukuu hizo.
Alisema jeshi la polisi tayari limeainisha njia ambazo watumia magari na watembea kwa miguu watazitumia wakati wa maadhimisho hayo na kuwataka watu watakaotumia maadhimisho hayo katika kuchoma ovyo matairi barabarani na kuziba njia kuwa watadhibitiwa.
“Kuzuaia barabara kwa kuchoma tairi ni kosa la jinai, hivyo tunawataka watu watakaojihusisha na vitendo hivyo, najua wanafanya hivyo kwa furaha ya kusherehekea sikukuu ya krismasi na mwaka mpya, lakini kusherehekea kwao kusiwe ni kero kwa watu wengine”, alisema.
Alisema kwa maadhimisho ya mwaka huu, jeshi la polisi limejizatiti kufanya doria maalum kwa kutumia magari, kuvaa sare za binafsi ili kuweza kuwabaini watu na wahalifu wenye lengo la kupora mali za wananchi.
“Polisi watakuwa kila mahali makanisani na barabarani ili kudhibiti hali ya usalama kwa wananchi, na kwa watu watakaoenda makanisani kusali nao watawekewa ulinzi wa maaskari ili wasiweze kuporwa”.
Aliwataka wananchi kutoa taarifa maalum pindi watakapoona watu wenye nia ya kuiba mali au kutaka kufanya uvamizi kwenye maeneo yao.