Na Abdulaziz Video, Lindi
Halmashauri ya wilaya ya Lindi, inaandaa taratibu za kuiburuza Mahakamani Gereji ya Auto Works Service ya Jijini Dar es salaam,kwa madai ya kuendelea kuishikilia gari yake, huku tayari ikiwa imeshalipwa fedha zote zilizokuwa ni ghalama za matengenezo yake.
Hayo yameelezwa na mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo, Grace Mbaruku,katika kikao cha kawaida cha Baraza la madiwani,lililofanyika hivi karibuni .
Mbaruku ametoa kauli hiyo,alipokuwa akijibu baadhi ya maswali kutoka kwa madiwani hao, waliotaka kufahamu hatua iliyofikiwa juu ya gari lao aina ya Toyota Cruser STJ 1826 iliyopelekwa gereji hiyo,kwa matengenezo na kuzuiwa na mzabuni huyo kwa zaidi ya miaka mitatu sasa akidai alipwe fedha zaidi.
Aliwaambia madiwani hao kwamba gari hiyo ilipelekwa gereji hiyo ya Auto Works Service kwa gharama ya Sh,19,446,400/-lakini matengenezo ambayo yamefanyika hadi kutembea yamefikia kiasi cha Sh,7,038,700/-ambacho tayari kimelipwa kupitia LPO Namba 001167.
“Kama ni fedha za matengenezo tayari ameshalipwa,lakini bado mzabuni huyu anaendelea kuizuia gari huku akitaka hadi alipwe Sh,19,446,400/-huku tayari fedha halali kwa kazi iliyofanyika ameshalipwa,,,,,,,,,,,sijui jeuri hii anaipata kutoka wapi?”Alisema Mbaruku.
Pia,mkurugenzi huyo mtendaji amesema kutokana na mzabuni huyo kuendelea kuishikilia gari hiyo hadi alipwe fedha hizo, Yaonesha anataka kuiibia Halmashauri yake kiasi cha Sh,12,407,700/-ikizingatiwa tayari imeshamlipa kulingana na kazi aliyokuwa ameifanya. Mkurugenzi huyo akasema kinachomsikitisha ni pale mzabuni huyo hataki kuikabidhi gari hilo,kwa madai kuwa bado anaidai fedha Halmashauri hiyo.
Akasema kutokana na kitendo cha mzabuni huyo kuendelea kuizuia gari hiyo,uongozi wa Halmashauri umeamua kuwasiliana na mwanasheria wake ili mzabuni huyo aweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Baada ya maelezo hayo,madiwani kwa kauli moja wamemtaka mkurugenzi huyo,kuharakisha taratibu za kuwasiliana na mwanasheria ili gari hiyo STJ 1826 likachukuliwe kwa Mwenye gereji hiyo haraka ili kusaidia shughuli za kiutendaji
Awali diwani wa kata ya Longa,Abdu Mjenga (CCM) aliitaka halmashauri hiyo kutoa taarifa kwa madiwani kuhusiana na gari hiyo iliyopelekwa kwenye gereji hiyo kwa muda mrefu bila ya wao kutopatiwa maendeleo na mrejesho wake huku wakijua imelipiwa matengenezo yake.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi Bi. Grace Mbaruku, akiongea katika kikao cha kawaida cha Baraza la madiwani,lililofanyika hivi karibuni .
Mmoja wa madiwani akichangia katika baraza hilo