Na Woinde Shizza,Arusha
Wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mererani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara wameiomba Serikali kuipatia leseni kampuni ya kizalendo ya Tan Youth Mining Ltd,ili wauziwe zana za milipuko kwa bei nafuu.
Wakizungumza leo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini chini ya Kaimu Mwenyekiti wake Anne Kilango Malecela,wachimbaji hao walisema kampuni hiyo ikipatiwa kibali na kufutiwa kodi watachimba madini kwa urahisi.
Mmoja kati ya wachimbaji hao,Sokota Mbuya alisema kampuni hiyo chini ya Mkurugenzi wake,Mohamed Karia ingepatiwa kibali cha kuwasambazia wachimbaji wadogo zana za milipuko wangekuwa na unafuu mkubwa.
“Kwanini mzalendo asipewe kibali cha kutusambazia zana,apewa mtu wa South Africa,ambaye hatusaidii chochote yaani inatusababisha twende hadi Nairobi Kenya kufuata zana za milipuko ya migodi,” alisema Mbuya.
Hata hivyo,Kamishna Msaidizi wa madini kanda ya kaskazini,Benjamin Mchwampaka aliieleza Kamati hiyo kuwa kwa alishaidhinisha kampuni hiyo ipatiwe kibali hicho,ila kinachokwamisha ni makao makuu wizarani.
“Kampuni hiyo ingeweza kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa suala la milipuko na nilishasaini yote yanayonihusu,ila wizarani bado hawajasaini na alishahojiwa mpaka na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa ,” alisema Mchwampaka.
Akizungumzia kuhusu hilo,Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo,Anne Kilango Malecela aliwataka wachimbaji hao kuandika barua kwenye kamati hiyo wakutane na wizara mwezi ujao ili kampuni hiyo ipatiwe kibali hicho.