Nyota wa mchezo wa mpira wa miguu wa Marekani(American Football) Rays Lewis akimpa RaisDkt. Jakaya Kikwete zawadi ya kofia yenye nembo ya timu yake wakati nyota huyo alipomtembelea Rais Kikwete mjini Arusha.Nyota huyo yuko nchini ambapo ni mmoja wa wafadhili wakubwa wa huduma kwa wagonjwa wenye ulemavu wa kusikia inayotolewa na taasisi ya Starkey Hearing Foundation ya nchini Marekani.Wagonjwa zaidi ya 3500 wanatarajiwa kunufaika na huduma hiyo inayotolewa bure na taasisi hiyo.
Muasisi wa Taasisi ya Strakey Hearing Foundation Bwana Bill Austin Starkey akimhudumia mtoto Lissa Frank(9) ambaye alikuwa kiziwi tangu kuzaliwa na kuweza kusikia baada ya kupata tiba na huduma ya kuwekewa kifaa maalumu katika kliniki maalumu iliyofanyika katika hospitali ya Seliani mkoani Arusha leo.
Waasisi wa Taasisi ya Starkey Foundation Bwana Bill Austin Starkey(kulia aliyeinama) na Mkewe Tani Austin(Wapili kushoto) pamoja na mhudumu kutoka hospitali ya Seliani(kushoto) wakifurahi baada ya mtoto Lissa Frank(9) kuweza kusikia vyema baada ya kupatiwa matibabu katika kliniki maalumu iliyofanyika katika hospitali ya Seliani mjini Arusha leo(picha na Freddy Maro)
====== ===== =========
WALEMAVU WA KUSIKIA WANUFAIKA NA HUDUMA ILIYOTOLEWA NA TAASISI YA STARKEY HEARING FOUNDATION.
Na.Freddy Maro,Seliani Arusha.
Julai, 7 ,2013.
Zaidi ya Watanzania 3500 wenye maradhi ya kusikia wanatarajiwa kunufaika kwa huduma ya tiba inayotolewa na Taasisi ya Starkey Hearing Foundation yenye makao yake jijini Washington nchini Marekani.
Muasisi wa Taasisi ya Starkey Hearing foundation Bwana Bill Austin Starkey ameyasema hayo wakati wa kliniki maalumu ya kuwatibu watu wenye maradhi mbalimbali ya kusikia iliyokuwa ikifanyika Katika hospitali ya Seliani mjini Arusha baada ya kutoa huduma hiyo katika miji ya Dar es Salaam na Moshi mkoani Kilimanjaro.
“Nimefurahishwa sana na kutiwa moyo kwa kazi tuliyoifanya ya kuwahudumia watu na kuwawezesha kusikia ambapo wengine ndiyo wameweza kusikia kwa mara ya kwanza tangu walipozaliwa.Furaha yao ni kitu cha kutia moyo sana katika juhudi zetu.Madaktari wa kitanzania tulioshirikiana nao wamefanya kazi kubwa na nzuri” alisema Bwana Starkey ambaye ameambatana na timu ya wataalamu na watu mashuhuri kutoka nchini Marekani ambao wametoa misaada mbalimbali kugharamia kampeni hiyo.
Bwana Starkey amesema kuwa watu wengi walijitokeza wakati wa kliniki hiyo maalumu kwa watu wenye ulemavu wa kusikia na kuongeza kuwa katika siku tatu walizokuwa mjini Arusha wagonjwa zaidi ya 600 walipatiwa huduma hiyo ya matibabu kwa kuwekewa vifaa maalumu katika masikio yako na kuwawezesha kusikia vyema na kusema kila mwaka shirika lake litafanya mipango ya kuhakikisha kwamba huduma hiyo inakuwa endelevu.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia wazazi wenye furaha baada ya kuona watoto wao wenye umri kati ya miaka mitano na kumi wakiweza kusikia vyema kwa mara ya kwanza katika maisha yao baada ya kupatiwa matibabu kwa kuwekewa vifaa maalumu katika masikio yao huduma ambayo imetolewa bure na shirika hilo na isingekuwa rahisi kuipata kwa watu wengi walio na kipato cha chini.
Bwana Bill Austin Starkey aliwashukuru wafadhili mbalimbali waliowezesha mpango huo wa matibabu kufanikiwa na kuongeza kuwa falsafa ya taasisi yake ni “Ili Dunia ipate kusikia” imeweza kutekelezwa kwa vitendo kwa sababu anaamini kuwa kukiwa na nia ya dhat na moyo wa kushirikiana kutekeleza jambo fulani mafanikio ni bayana na mabadiliko mengi chanya yatawezekana katika ulimwengu.
Bill Austin Starkey na mkewe Tani Austin ambaye ni muasisi mwenza wa taasisi hiyo pamoja na washirika wao wanatarajia kwenda nchini Malawi kutoa huduma kama hiyo na baadaye kurejea tena nchini kutoa huduma kabla ya kuondoka kurejea nchini marekani.
Mmoja wa wataalamu wanaotoa huduma katika kliniki hiyoDkt. Ron Brouillete alisema mbali na kuzaliwa na ulemavu wa kutosikia wangojwa wengine waliotibiwa katika kliniki hiyo walipata madhara ya kutosikia kutokana na matumizi holela ya dawa ya kutibu Malaria aina ya Quinine.
“Napenda kutoa ushauri kwa madaktari na wahudumu katika sekta ya afya kuepuka kuwapa dawa ya Quinine wagonjwa wa Malaria.Dawa hii itumike kwa uangalifu mkubwa na pale ambapo dawa nyingine zimeshindwa kumtibu Mgonjwa,” alisisitiza mtaalamu huyo kutoka nchini Marekani .
Mmoja wa wafadhili wa mradi huo anayefuatana na Bwana Bill Austin Starkey ni mcheza mpira wa miguu maarufu wa Marekani(American Professional Football) Bwana Ray Lewis ambaye pia anachezea ligi ya taifa ya mpira wa miguu ya nchi hiyo(National Football League).
Awali Mchezaji huyo alimtembelea Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete aliyekuwa mapumzikoni mjini Arusha na kusema kuwa Rais Kikwete ni mmoja kati ya viongozi mashuhuri barani Afrika wenye maono ya mbali na nia ya dhati ya kuwahudumia wananchi wake.
“Nimesoma habari nyingi mambo mangi yenye mafanikio makubwa anayoyafanya Rais Kikwete na nilipopata fursa ya kuja nchini Tanzania nikatumia nafasi hiyo kuja kumsalimia,kumsikiliza na kumpongeza.Ni mtu mnyenyekevu sana na nimefurahi sana kumtembelea na kuongea naye,” alisema nyota huyo wa mpira wa miguu Marekani muda mfupi baada ya kukutana na Rais Kikwete ambapo alimzawadia kofia yenye nembo ya timu yake.
Bill Austin Starkey na mkewe Tani Austin waliunda Taasisi ya Starkey Hearing foundation mwaka 1984 kwa lengo la kusaidia watu wenye maradhi ya kusikia na mpaka sasa maelfu ya watu katika sehemu mbalimbali duniani wamenufaika na huduma inayotolewa na taasisi hiyo.