Mpango wa Afrika Kujithmini Kiutawala Bora (APRM) umesema kuwa Serikali ya Tanzania imeanza kutekeleza maoni ya wananchi yaliyotolewa kwa nyakati mbalimbali nchini na kuingizwa katika ripoti ya Mpango huo.
Maoni hayo yalihusu masuala ya katiba, siasa demokrasia, namna nchi inavyosimamia uchumi na pia wananchi wengi walizungumzia masuala ya upanuaji wa huduma za kijamii kama afya, elimu na nishati uwekezaji na migogoro mbalimbali.
Akizungumza kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa APRM Tanzania, Bw. Hassan Abbas alisema ingawa ripoti hiyo itazinduliwa rasmi hivi karibuni, tayari baadhi ya masuala yameanza kufanyiwa kazi na Serikali.
“Ripoti yetu ya APRM baada ya Rais Jakaya Kikwete kuiwasilisha kwa wakuu wenzake wa APRM Januari mwaka huu hivi sasa inasubiri kuzinduliwa rasmi. Hata hivyo tayari Sekretarieti ya APRM Tanzania ilipeleka baadhi ya masuala yaliyomo na kuingizwa katika baadhi ya Bajeti za Serikali.
“Pia masuala yote yanayohusu Katiba yaliwasilishwa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kote huko tumeona masuala kadhaa ya msingi kutoka Ripoti ya APRM yamefanyiwakazi,” alisema Bw. Abbas.
Kwa mujibu wa Bw. Abbas kabla na hata baada ya uzinduzi huo miongozo ya uendeshaji ya APRM imeainisha kuwa ni muhimu kuwapa mrejesho wananchi walioshiriki katika kuishauri Serikali yao.
“Kwa hiyo tunaandaa namna ya kuhakikisha tunawapa mrejesho wananchi wote walioshiriki zoezi la awali na hata ambao hawakushiriki ili wafahamu masuala ya msingi yaliyoingizwa kwenye Ripoti ni yapi ili nao wafuatilie utekelezaji wa masuala hayo kadiri Serikali inapokuwa inafanya hivyo,” aliongeza.
Aliongeza kuwa utafiti wa APRM umehusisha wananchi na wataalamu ambapo maoni yalitolewa katika maeneo makuu manne ya utafiti ambayo ni demokrasia na utawala bora katika siasa; utawala bora katika mashirika ya umma; utawala bora katika uendeshaji wa makampuni na utoaji wa huduma za kiuchumi na kijamii.
Akieleza chimbuko la APRM, Bw. Abbas alisema kuwa ni mpango endelevu uliobuniwa na viongozi wa Afrika katika kikao chao cha mwaka 2003 ambapo walikubaliana kuweka utaratibu wa kila nchi kuanzisha taasisi hiyo na kisha kuipa jukumu la kufanyakazi ya kujitathmini mara kwa mara katika nyanja za utawala bora.
Bw. Abbas aliongeza kuwa kwa mujibu wa Mkataba huo wa Afrika, APRM sio kitu cha mara moja, ni taasisi yenye malengo ya kudumu ambapo kila nchi iliyojiunga itaendelea kuwa ikitathminiwa kila baada ya miaka minne.
Taarifa zinaoneshan kati ya nchi 33 za Umoja wa Afrika zilizojiunga na APRM, tayari nchi za Kenya, Rwanda, Ghana na Nigeria zilikwishakamilisha tathmini ya mwanzo na sasa zinajiandaa kufanyiwa tathmini ya pili ili kubaini changamoto mpya na kuzifanyikakazi.