Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe (katikati) akiwa pamoja na baadhi ya wageni wa meza kuu wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa tano wa mwaka wa Bodi za Maji za Mabonde leo jijini Mbeya. Kulia kwa Waziri wa Maji ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe.Abbas Kandaro.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Abbas Kandoro akitoa taarifa rasmi ya hali ya Maji Mkoani Mbeya kwa wajumbe wa Mkutano watano wa mwaka wa Bodi za Maji za Mabonde (hawamo pichani) jijini Mbeya leo asubuhi.
Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe akifungua rasmi Mkutano wa tano wa mwaka wa Bodi za Maji za Mabonde leo jijini Mbeya.
Baadhi ya wadau wa sekta ya maji wanaoshiriki Mkutano wa tano wa mwaka wa Bodi za Maji za Mabonde ulioanza leo jijini Mbeya.
Wadau wa sekta ya maji wanaoshiriki katika Mkutano wa tano wa mwaka wa Bodi za Maji za Mabonde wakiwa katika picha ya pamoja leo jijini Mbeya.
===== ====== ======
WAZIRI WA MAJI AFUNGUA MKUTANO WA MWAKA WA BODI ZA MAJI ZA MABONDE JIJINI MBEYA.
Waziri wa Maji Pro.Jumanne Maghembe amefungua Mkutano wa tano wa mwaka wa Bodi za Maji za Mabonde leo jijini Mbeya katika ukumbi wa Hoteli ya Mtenda Sunset and Conference Centre.
Katika mkutano huo, Prof. Maghembe alisisitiza kuweka mkakati wa utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla, kwa kuandaa mpango maalum wa taifa wa utunzaji wa vyanzo vya maji wa miaka mitano.
Pia, alishauri kuanzisha Mfuko wa Vyanzo vya Maji kwa ajili ya jamii zinazoishi karibu na vyanzo hivyo, maalum kwa kuwezesha utunzaji wa vyanzo hivyo ili kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa kwa ufanisi mzuri. Na akapendekeza kiasi cha Sh. bil. 3-5 kwa kuanza mfuko huo.
Lengo la mkutano huu ni kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya maji ili kupitia utekelezaji wa malengo na mikakati katika usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji kwa nia ya kuhakikisha kuwa rasilimali hizo zinatumika kwa uwiano mzuri kwa sekta zote na kwa njia endelevu. Kauli mbiu ya mkutano wa mwaka huu ni “Jitihada za Pamoja katika Kutunza na Kulinda Vyanzo vya Maji ni Muhimu ili Kuhakikisha Upatikanaji wa Maji.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mha. Bashir Mrindoko, aliongeza kuwa anategemea mbinu zaidi zitatumika katika kutekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji , ikiwemo njia ya usimamizi shirikishi ili kupata ufumbuzi wa changamoto hizo.
Mkutano huo unategemea kuendelea mpaka tarehe 5, Julai na utahusisha pia kutembelea vyanzo vya maji mkoani Mbeya, ambapo kunapatikana karibu 70% ya vyanzo vya maji nchini.