Leo asubuhi Balozi Wilfred Joseph Ngirwa amepokelewa kwa shangwe na bashasha alipoketi rasmi, kwa mara ya kwanza, kwenye kiti chake tayari kufungua na kuendesha Kikao cha 147 cha Baraza la FAO.
Balozi Ngirwa alianza kwa kuwashukuru wanachama wote wa FAO kwa kumchagua kwa asilimia 95 kwenye Mkutano Mkuu wa 38 wa FAO hapo tarehe 21 Juni, 2013 na baadaye kumteua rasmi kwenye nafasi hiyo ya Mwenyekiti wa Baraza la FAO (Independent Chairperson of the FAO Council) hapo tarehe 22 Juni, 2013 kama taratibu na kanuni zinavyotaka.
Balozi Ngirwa aliahidi kuitumikia nafasi hiyo kwa uaminifu na kujituma, akiweka mbele maslahi na malengo ya FAO. Aidha, Balozi Ngirwa aliomba ushirikiano kutoka kwa Wajumbe wa Baraza, na nchi wanachama wote wa FAO kwa ujumla.
Katika mahojiano yetu awali, Balozi Ngirwa alimshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dr. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa imani kwake na hata kukubali Tanzania impendekeze, kama kanuni zinavyotaka, kama mgombea wa nafasi hiyo.
Aidha, alimshukuru kwa dhati Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Ben Membe (MP), na Wizara yake kwa ujumla, kwa kampeni nzuri na za mafanikio makubwa. Pia alimshukuru sana Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhe. Eng. Christopher K. Chiza (MP), pamoja na Wizara yake kwa juhudi za hali na mali hadi kupatikana kwa ushindi.
Pamoja na shukrani kwa wengine wengi, Balozi Ngirwa alimshukuru Balozi na Watumishi wote wa Ubalozi wa Tanzania Roma kwa kujitolea kwa dhati kufanya kampeni pevu katika anga za kidiplomasia kwa kipindi chote cha miezi 14 tangu jina lake lilipopendekezwa kwa mara ya kwanza katika duru za FAO na kufungua mlango wa kuungwa mkono na makundi yote, kuanzia na kundi la Africa (FAO Regional Group for Africa) kwenye Mkutano uliofanyika huko Congo-Brazzaville mwezi April, 2012.
Aliahidi kutoa ushirikiano wa dhati kwa Ubalozi katika kipindi chote cha uwepo wake kwenye nafasi hiyo, pia akitegemea ushirikiano wa Ubalozi wa Tanzania Roma kumwezesha kutekeleza vyema majukumu yake.
Balozi Ngirwa anakuwa mwafrika wa pili kuchukua nafasi hiyo tangu mwaka 1945 wakati lilipoanzishwa Shirika hili la Chakula la Umoja wa Mataifa. Balozi Ngirwa, mtaalam wa masuala ya kilimo na chakula, ana uzoefu mkubwa kupitia utumishi wake uliomfikisha hadi ngazi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo nchini Tanzania. Baadaye aliteuliwa na Mhe. Rais kuja Roma kama mwakilishi wetu wa kudumu kwenye mashirika ya chakula ya Umoja wa Mataifa, ambapo alipata pia uzoefu mkubwa katika diplomasia kwa miaka 6, hadi alipostaafu mwezi Machi, 2012.
Ni matumaini yetu kuwa Watanzania tutampa ushirikiano na kumsaidia kuiwezesha Tanzania kufaidika na kuendeleza vyema maslahi yake katika mashirikiano na mashirika haya ya Umoja wa Mataifa jijini Roma.
Balozi Ngirwa akiendesha Mkutano wa 147 wa Baraza la FAO uliofunguliwa leo asubuhi. Pembeni yake ni Katibu Mkuu wa Baraza na Mkutano Mkuu wa FAO.
Wajumbe na wahudhuriaji (observers) wa kikao cha 147 cha Baraza la FAO leo asubuhi katika Red Room, makao Makuu ya FAO.
Balozi Eng. Dr. James Alex Msekela (wa pili kulia walioketi) akiwa na Mwambata Kilimo na msaidizi wake Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyopo Roma, Bw. Ayoub Mndeme, wakishiriki kwenye kikao cha 147 cha Baraza la FAO leo asubuhi.