Na Othman Khamis Ame
Timu zipatazo 13 za Mchezo wa Soka za Kitaifa na Kimataifa zinatarajiwa kushiriki katika mashirndano ya Kombe la Mapinduzi yanayotarajiwa kufanyika ndani ya kipindi cha Maadhimisho ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 2014. Hayo yamejiri wakati Uongozi wa Kamati ya Mapinduzi Cup ulipokutana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kumpatia taarifa kufuatia hatua za awali za maandilizi ya mashindano hayo yanayotarajiwa kuwa ya Kimataifa.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Sharifa Khamis alimueleza Balozi Seif kwamba Kamati hiyo imezingatia agizo la Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohd Sheni la kuzialika pia kwenye mashindano hayo Timu za Soka za China, Vietnam na Oman kutokana na uhusiano mzuri uliopo baina ya Zanzibar na Nchi hizo. Sharifa alizitaja baadhi ya timu nyengine zitakazoalikwa katika mashindano hayo kuwa ni pamoja na Yanga, Simba na Azam za Tanzania Bara, Tasker ya Kenya, URA ya Uganda, APR ya Rwanda na wenyeji wa mashindano hayo timu za KMKM,Jamuhuri na Chuoni.
“ Kamati yetu imeamua kuanza mapema maandalizi hayo kutokana na umuhimu wa sherehe zenyewe na kikao chetu cha kwanza tumefikia hatua za kufikiria njia za kupata fedha za maandalizi pamoja na timu tutakazozialika kushiriki mashindano hayo “. Alifafanua Sharifa Khamis.
Alieleza kwamba mashindano hayo yanatarajiwa kupangwa katika mfumo wa makundi mawili Unguja na Pemba ili kuwapa fursa wapenzi wa michezo kisiwani pemba kuona mashindano hayo. Naye mjumbe wa Kamati hiyo ambae pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni, Utalii na Michezo Dr. Ali Mwinyikai alisema Kamati hiyo pia imefikiria kushirikisha michezo ya Pete pamoja na Riadha ili kuongeza vugu vugu la mashindano hayo.
Dr. Mwinyikai alieleza kwamba Kamati hiyo imeanza hatua za kuwasiliana na baadhi ya wadau wa michezo ndani na nje ya Nchi katika hatua ya kuona mashindano hayo yanafanyika kwa mafanikio makubwa kulingana na maadhimisho yenyewe.
Katika kukifanyia maandalizi ya mapema kiwanja cha michezo cha Amani Mwinyikai alisema Kamati hiyo kwa kushirikiana na Wizara inayosimamia michezo Zanzibar wamefikiria kukiwekea nyasi bandia kiwanja hicho ili kiwahi kutumika katika mashindano hayo ya Mapinduzi Cup.
Alisema Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo imeweka kifungu maalum kitakachounga mkono kazi hiyo ndani ya makadirio ya Mapato na Matumizi yake kwa mwaka wa fedha endapo kitapita katika kikao cha baraza kinaoendelea.
Akitoa shukrani zake kwa hatua iliyofikiwa na Kamati hiyo kwa kuanza vizuri maandalizi hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na yeye binafsi itajitahidi kuunga mkono Kamati hiyo ili ifikie lengo iliyojipangia. Balozi Seif aliihakikishia Kamati hiyo kwamba atachukuwa jitihada za ziada katika kuona wale wadau, Mashirika na hata Taasisi zinazofikiriwa kuunga mkono harakati hizo kimawazo na hata uwezeshaji wanasaidia.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhimiza Uongozi wa Kamati hiyo ya Mapinduzi Cup kuendelea na maandalizi katika hatua kubwa na makini ili kuona lile kusudio la kufanikisha mashindano hayo muhimu linafikiwa.
“ Katika kulipa nguvu za himizo la ziada suala hili nitakuombeni kwa hatua zinavyosonga mbele ni vyema tukakutana tena mwishoni mwa mwezi wa Julai ili kuangalia tumefikia hatua ipi na tumekwama wapi katika Maandalizi hayo “. Aliagiza Balozi Seif.
Mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanayofanyika mnamo Mwezi wa Januari kila mwaka mara hii fainali yake imepangwa kufanyika siku ya Pili ya Maashimisho ya Sherehe za Mapinduzi Januari 12 ambayo itakuwa Tarehe 13 Januari 2014.
Uamuzi huo umechukuliwa na Kamati hiyo ili kuwapa nafasi nzuri Wananchi na wapenzi wa Michezo na sanaa kushiriki katika matukio yote yanayoambatana na sherehe hizo ikiwemo burdani na muziki wa Taarabu uliozoeleka kufanyika usiku wa kilele cha sherehe hizo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiipongeza Kamati ya Mapinduzi Cup aliyokutana nayo kuangalia hatua wanazochukuwa katika maandalizi ya Mashindano ya kombe hilo ambapo maadhimisho ya Sherehe za Mapinduzi zinafikia nusu Karne (miaka 50)
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mapinduzi Cup Sharifa Khamis akielezea hatua inazoendelea kuchukuwa Kamati yake katika maandalizi ya mashindao hayo ambayo mara hii yanatarajiwa kuwa ya Kimataifa.
Mjumbe wa Kamati ya Mapinduzi Cup ambae pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Dr. Ali Mwinyikai akifafanua Mikakati iliyojipangia Kamati hiyo katika kutafuta fedha za kufanikisha mashindano ya Mapinduzi Cup.
Moja kati ya mikakati hiyo ni kuhakikisha uwanja wa michezo wa Amani unawekewa nyasi bandia ili kuuwezesha uwanja huo kuhimili mashindano hayo.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.