Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Almas Kassongo (kushoto) akimkabidhi Sh 500,000, Meneja wa Friends Rangers, Shaaban Marsila mara baada ya timu hiyo kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa.
TIMU ya Friends Rangers ya jijini Dar es Salaam imetamba kuibuka na ushindi dhidi ya Stand United ya mkoani Shinyanga katika mechi ya Ligi ya Mabingwa (RCL) itakayochezwa kesho Juni 23 kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi.
Akizungumza leo hii Juni 22, Meneja wa Friends Rangers, Shaaban Marsila alisema wamejipanga vyema kuhakikisha wanashinda mechi hiyo ili iwe rahisi kwao katika mechi ya marudiano itakayochezwa Juni 30.
“Kikubwa mabacho naweza kusema ni kwamba timu imendaliwa vizuri kwa ajili ya kushinda na mechi dhidi ya Stand United, tunaamini tukishinda mechi hiyo itakuwa rahisi kwetu katika mechi ya marudiano.
“Tunawaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kwenye Uwanja wa Azam Complex kuishangilia kwa nguvu timu yao ili ipate ushindi,” alisema Marsila.
Friends Rangers ndio timu pekee iliyosalia katika ligi hiyo ya mabingwa kutoka jijini Dar es Salaam huku timu za Abajalo na Red Coast zikiaga mashindano hayo ambayo timu tatu zitafuzu kucheza Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.
Katika kuelekea katika mechi hiyo, tayari Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), kupitia kwa Ofisa Habari wake, Mohamed Mharizo kimeitakia kila la kheri Friends Rangers ili iweze kuibuka na ushindi dhidi ya Stand United.
“Kwa niaba ya DRFA nachukua fursa hii kuwatakia kila la khri Friends Rangers katika mechi hiyo, kwani wamekuwa wawakilishi wetu wazuri na naamini wataendelea kutuwakilisha vyema,” alisema Mharizo.