Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Angella Kairuki (mwenye koti la pink) akimsikiliza Bw. Paschal Mayumba Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mvumi Makulu anayehudumia Mahakama ya Mwanzo Mvumi Makulu na Mahakama ya Mwanzo ya Handali akitoa ufafanuzi wa jambo kuhusu kiwanja ambacho Mahakama ya Mwanzo ya Handali imepewa na Uongozi wa Kijiji kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Mahakama hiyo. Kushoto kwa Mhe. Kairuki ni Mhe. Livingstone Lusinde, Mbunge wa Jimbo la Mtera, ambaye aliambatana na Naibu Waziri katika kutembelea Mahakama za Mwanzo za Wilaya ya Chamwino. Wengine katika picha hiyo ni viongozi wa Mahakama na viongozi wa Serikali ya Kijiji cha Handali.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Angella Kairuki akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Makang’wa Wilayani Chamwino na kuwahamasisha kujenga majengo ya Mahakama kwa nguvu zao ili waweze kupata huduma hii muhimu karibu na maeneo yao na kuacha kutembea umbali mrefu kuzifuata mahakama ili kupata haki zao. Aidha,Mhesjhimiwa Kairuki aliwaahidi wananchi hao kwamba Serikali kupitia Mahakama itashirikiana nao katika kujenga jengo la Mahakama katika eneo hilo.
Mbunge wa Jimbo la Mtera, Mhe. Livingstone Lusinde akiuelezea ujumbe wa Mhe. Angellah Kairuki namna ambavyo uongozi wa Mahakama umepewa kiwanja na uongozi wa Kata ya Mvumi Mission kwa ajili ya ujenzi wa jengo jipya la Mahakama ya Mwanzo. Hadi sasa eneo hilo lenye wakazi wengi halina huduma ya Mahakama na hivyo kuwalazimu wananchi wa eneo hilo kutembea umbali mrefu kutafuta haki zao.