Salamaleko Ankal Michuzi na Timu nzima ya Globu ya Jamii.
Ama baada ya salamu,naomba unipandishie kwenye Globu ya Jamii hoja yangu hii kuhusiana na utaratibu wa ulipiaji wa maegesho ya magari katika Uwanja wa Ndege wa zamani (Terminal 1) jijini Dar es Salaam.
Maana hivi karibuni nilikuwa nimeenda uwanjani hapo kumsindikiza ndugu yangu,nilipofika getini nikamkuta jamaa kakaa kwenye kiti huku akiwa ameshika kamba iliyokuwa kwenye chuma lililokuwa limefunga njia na nilipokaribia kwenye chuma lile,jamaa huyo akanyanyuka kwenye kiti chake na akaja dirishani na kunipatia kikadi hicho pichani (si kama kule Terminal 2 ambako tunachukua kwenye mashine) kwa ajili ya kuonyesha muda wa kuegesha gari katika Maegesho ya uwanjani hapo,nikamuuliza kuwa na huku mnachukua ushuru wa Maegesho ya magari?akanijibu ndio na gharama zake ni kama zile za kule Terminal 2.
Sikuwa na maswali mengi zaidi,nikachukua kikadi hicho na kuendelea na safari yangu.
Nilifika sehemu nikaegesha gari na kwenda na yule ndugu yangu mpaka sehemu ya kukata tiketi na baada ya kupata,tukakaa kidogo kupiga stori mbili tatu wakati tukisubiri muda wa safari yake ukaribie ili tuweze kuagana na mie niondoke zangu.
Baadae muda wa safari ukawadia kwa ndugu yangu na mie ndio ukawa muda muafaka wa kuondoka uwanjani hapo,kabla sijaelekea kwenye gari nikakumbuka kuwa nilipewa kikadi cha Maegesho ya gari na hapo ndipo nilipo papasa macho kushoto na kulia ili nione sehemu ya kulipia na kwa bahati nzuri nilikiona kibanda kidogo cheupe (picha ya chini) chenye bango la njano linalotoa maelezo kuwa ni sehemu ya kulipia maegesho hayo.
Nikaenda mpaka pale na kumkuta mwanadada mrembo mwenye tabasamu la kumtoa nyoka pangoni,nikampatia kile kikadi nae akakiangalia na kuniambia natakiwa kulipia shilingi elfu tatu (3,000/=) kwa hesabu alizozipiga kupitia kalukuleta iliyokuwepo mezani pale.
Nikatoa noti ya Shilingi elfu tano nikampatia na yeye akanirudishia shilingi elfu mbili na hicho kikadi akiwa amekiandika tu na peni muda wa kuondoka.
Hapo ndipo nilipomuuliza yule dada kuwa Risiti iko wapi??akanijibu kuwa bado hawajaanza kutoa risiti katika maegesho ya uwanja huo.Nikamuuliza tena inamaana watu wote mnawafanyia hivi,akanijibu ndio wanafanya hivyo toka wameanza kutoza ushuru katika sehemu hiyo.
Sasa hapo ndipo nilipopatwa na Maswali mengi kichwani kuwa hela inayotozwa katika maegesho hayo inakwenda wapi??na inafayiwa kazi gani??na kwanini utaratibu wao ni mbovu namna hiyo?? na maswali mengine mengi bila ya majibu.
Nikaona isiwe shida nikaondoka zangu na leo ndio nimeona nikuletee wewe Ankal ili uiweke kwenye Libeneke letu la Globu ya Jamii ili wadau waweze kuchangia maoni yao na ikiwezekana swala hili lifanyiwe kazi na kuondoa kabisa mambo hayo yanayoendelea katika Maegesho hayo.
Ahsante.
-Mdau wa Globu ya Jamii
Jijini Dar.