Na Bashir Yakub.
Ndio ni kweli mwanamke aliyeolewa anaweza kukopa hela kwa jina la mme wake. Tena kukopa kwenyewe si lazima awe amepata ridhaa au ruhusa kutoka kwa mme wake.
Pia si ruhusa tu bali si lazima amtaarifu mme huyo. Sheria ya ndoa , sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 ndiyo iliyoeleza jambo hili . Lipo kifungu cha 64 cha sheria hiyo.
Kwa ujumla makala haya yatatizama jambo hili likoje, linahusisha nini na nini, vigezo na sifa za kufanya hivyo na mambo mengine ambayo yanalizunguka jambo hili lakini kwa ufupi.
1.MWANAMKE GANI ANAWEZA KUKOPA.
Kifungu hicho kimesema mwanamke anayeweza kukopa ni yule aliye kwenye ndoa inayotambulika kisheria. Ikiwa mwanamke hayupo katika ndoa ambayo sheria inaitambua basi haki hii ya kukopa kwa jina la mme wake anaikosa.
Ikiwa mmetengana lakini ndoa haijavunjika kisheria basi haki hii inaendelea kubaki. Isipokuwa tu itaondoka ikiwa mmetengana kwa makubaliano maalum ambapo matunzo na matumizi yote mwanamke anapata bila wasiwasi.
Pia ikiwa kuna talaka basi mwanamke hawezi kukopa kwa jina la mme wake kwa kuwa talaka kisheria inavunja ndoa na hivyo tafsiri yake ni kuwa hakuna ndoa. Lakini kukiwa na shauri la talaka mahakamani na ndoa haijavunjwa rasmi na mahakama basi haki hii inaendelea kubaki kwa mwanamke huyo.
2. KWANINI SHERIA IMEMRUHUSU MWANAMKE KUKOPA KWA JINA LA MME .
Sheria imemruhusu mwanamke kukopa kwa jina la mme wake tena bila hata ridhaa ya mme wake kwakuwa imempa wajibu mume kumtunza mke wake na mtoto/watoto kama yupo. Kwa mujibu wa sheria ya ndoa ni lazima mume kumtunza mke wake pamoja na watoto kama wapo.
Kwa upande mwingine mwanamke naye anaruhusiwa kumtunza mme wake lakini kwake sio lazima. Sheria haijampa ulazima mwanamke bali mwanaume . Kwahiyo ni katika mazingira haya ambapo suala la mke kukopa bila ridhaa ya mme wake tena kwa jina la mme huyo linapokuja.
Hata hivyo sio wakati wote mwanamke anaruhusiwa kukopa kwa njia hiyo bali ni pale tu mume wake anapokaidi wajibu wake wa lazima wa kumpa matunzo/matumizi. Hapa ndipo mwanamke anaweza kukopa kwa jina la mme wake tena bila hata ridhaa ya mme huyo.
Mke hataruhusiwa tu kufanya hivyo kwa kutopewa mahitaji yake pekee bali pia hata kama ana watoto/mtoto nao hawajapewa mahitaji basi hata hapo anaruhusiwa kukopa.
KUSOMA ZAIDI sheriayakub.blogspot.com