Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini kwa kushirikiana na Chuo cha Sokoine cha Kilimo (SUA) chini ya ufadhili wa shirika la ‘Climate Change Agriculture and Food Security CCAFS’ linalotekeleza mradi wa elimu ya asili katika utoaji wa utabiri wa hali ya hewa katika wilaya ya Lushoto.
Akizungumza katika uzinduzi huo,Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania , Dkt Agnes Kijazi alisema utekelezaji wa mradi huu ulianza Agost 2012 na unatarajiwa kuisha mwezi Desemba 2013 ambapo watabiri wa asili wapatao 27 wamehusishwa.
Dkt Kijazi alisema kwa vile wilaya ya Lushoto hupata misimu miwili ya mvua kwa mwaka yaani Vuli na Masika, watabiri hao waasili walihusihwa katika kutoa utabiri wa Vuli 2012 na Masika 2013, na kubaini kushabihiana kwa kiasi kikubwa kwa utabiri wa kisayansi uliotolewa na TMA pamoja na ule wa asili, viashiria vya asili vinavyotumika ni pamoja na wadudu,mimea,wanyama na upepo.
Aliendelea lusema katika kuhakikisha kwamba utabiri wa hali ya hewa unawafikia wakulima kwa wakati ndipo TMA na SUA wameanzisha mfumo wa FarmSMS ambapo uendeshwaji wake utakuwa TMA.
Akizundua rasmi mfumo huo, Kwa niaba ya MKuu wa Wilaya ya Lushoto Bwana Charles Moshi aliwashukuru TMA pamoja na SUA kwa kuwakumbuka wakulima wa Wilaya yake, kwa vile Wilaya ya Lushoto ni moja ya eneo lililoathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi kwa kupata upungufu wa mvua katika maeneo mengi, hivyo natarajia kwa mfumo huu wakulima wataweza kupata taarifa sahihi na kwa wakati, Bw. Moshi alisema wazee wa lushoto wamekuwa wakitoa utabiri wa hali ya hewa kwa njia ya asili tangu zamani, ni faraja yetu kuona sasa watabiri wa asili wataweza kuungana na watabiri wa kisayansi katika kutoa utabiri wa eneo husika katika wilaya yetu, hali hii isaidia kuweka kumbukumbu za viashiria vya asili vya utabiri wa hali ya hewa kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Aliendelea kuwashukuru wa TMA kwa kuweka kituo cha hali ya hewa kinachojiendesha chenyewe (Automatic Weather Station) katika Wilaya yake na kuahidi kuwa uongozi wa wilaya ya Lushoto utahakikisha matokeo ya utafiti yanakuwa endelevu Akizungumza kwa niaba wa wazee wa asili na wakulima wa Wilayani Lushoto,Bw. Benard alisema kutokana na mabadiliko ya tabia nchi baadhi ya viashiria vinapotea hivyo kwa kushirikiana na utabiri wa kisayansi hii itasaidia wakulima kujua hali ya hewa sahihi na pia kuwepo kwa kumbukumbu kwa vizazi vijavyo.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini kwa kushirikiana na SUA kupitia msimamizi wa mradi Profesa Henry Mahoo wamezindua rasmi huduma ya FarmSMS ambapo mkulima ataweza kupata utabiri wa hali ya hewa, ushauri na tahadhari za hali ya hewa kupitia simu ya mkononi.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt.Agnes Kijazi akifafanua jambo kwa wakulima na watabiri wa asili.
Baadhi ya wakulima na watabiri wa asili wakifuatilia uzinduzi wa FarmSMS.
Bw.Edwin Ligenge, mtaalam kutoka TMA akieleza jinsi ya kujiunga na huduma ya FarmSMS.
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Bw. Charles Moshi(wa tano kutoka kulia mstari wa mbele), Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi( wan ne kutoka kulia mstari wa mbele), Msimamizi wa mradi na mwakilishi kutoka SUA Prot. Mahoo (wa pili kutoka kushto mstari wa mbele) katika picha ya pamoja na wataalam kutoka TMA, SUA na watabri wa asili na wakulima.