


BENKI ya NMB imekutanisha wafanyabiashara zaidi ya 500 wa jijini Dar es Salaam waliopo katika jumuia ya wafanyabiashara wa NMB "NMB Business Club" kwa lengo la kutoa mafunzo mbalimbali ya biashara pamoja na mafunzo ya kodi ili kukuza biashara zao.
Kundi hilo la NMB Business Club mkoa wa Dar es Salaam limekutanishwa kwa pamoja ili wafanyabiashara hao waweze kujuana na kubadilishana uzoefu katika shughuli zao jambo ambalo litachangia wao kushikamana na kunufaika zaidi na huduma zinazotolewa na benki hiyo.
Akizungumza na wafanyabiashara katika mkutano huo, Afisa Mkuu wa NMB Kitengo cha Wateja wadogo na wakati, Abdulmajid Nsekela alisema katika semina hiyo wataalam wa biashara wa Benki ya NMB watatoa mafunzo mbalimbali ya namna ya kukuza biashara na kuelezea fursa anuai zilizopo ndani ya benki hiyo ili wateja wao waendelee kunufaika nazo. Alisema mbali ya kutoa mafunzo ya biashara na kodi wana NMB Business Club walioshiriki katika mkutano huo watapata fursa ya kutoa mrejesho dhidi ya huduma wanazopewa ili benki iangalie namna ya kuzishughulikia.
Sehemu ya wafanyabiashara walioshiriki mkutano huo.
