Na Tiganya Vincent-RS-Tabora
Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Dkt. Thea Ntara ametoa wito kwa wanawake mkoani hapa kuungana na kushirikiana pamoja katika shughili za mbalimbali za ujasiriamali ili iwe rahisi kwao kunafaika na fursa mbalimbali mikopo ikiwemo asilimia tano inapaswa kutolewa na Halmashauri zao.
Dkt. Ntara alitoa kauli hiyo jana mjini Tabora wakati akizindua Jukwaa la Uwezeshaji wanawake kiuchumi la Mkoa huo.Alisema kuwa wanawake wakiendelea kufanyakazi kwa ubinafsi hawataweza kuendelea bali wataendelea kubaki nyuma.
Katibu Tawala huyo wa Mkoa alisema kuwa wanawake wakiungana na wakaunda vikiundi vinavyoaminika watapata fursa ya kukopeshwa na Taasisi za fedha zilizopo mkoani Tabora na hivyo kukuza mitaji yao ambapo hatimaye wanaweza kuwa na uwezo wa kuanzisha viwanda vyao.
Dkt. Ntara aliongeza kuwa wakiungana watapata fursa ya wao kuwa kichocheo cha kuleta maendeleo kuanzia ngazi za familia hadi taifa kutokana na wao kuwa wataalam wazuri wa matumizi ya fedha kidogo wanazopata.
Alisema kuwa mwanamke licha ya baadhi yao kutokwenda shule au kutopata fursa ya kusoma lakini bado Mungu amewajalia maarifa ambayo yanasaidia jamii kama vile kufahamu kuwa mtoto wake anaumwa wakati hajasomea udaktari, kufahamu umuhimu wa kilimo cha mboga mboga kuzungumza nyumba yake licha ya kutosomea ubwana au ubibi shamba, kuwa mtunza fedha mzuri licha ya kutosomea uhasibu.