Mahmoud Ahmad, Arusha
Serikali imewapeleka nchini Kenya Vijana wawili waathirika wa mlipuko wa mabomu juzi Arusha kwenda kupatiwa matibabu zaidi kwenye hospital ya Agakhan ya jijini Nairobi.
Mkuu wa mkoa waArusha Mhe Magessa Mulongo amesema leo kuwa kutokana na maombi ya mama wa watoto hao na kujali wananchi wake serikali imeamua kuwapeleka watoto Sharifa na Fatuma Jumanne nchini Kenya kwa matibabu zaidi.
Mhe Mulongo alisema kuwa kutokana na ripoti ya madaktari wa hospitali ya Selian na hali za vijana hao kuwa mbaya, serikali imeamua kugharamia matibabu ya majeraha kwenye viungo vyao vya mwili na Kichwa.
Alisema kuwa timu ya madaktari wa mifupa kutoka Hospitali ya Muhimbili kitengo cha mifupa cha MOI tayari wapo jijini hapa kuungana na madaktari wa hospitali za Selian na hospital ya mkoa Mount Meru kuendelea na matibabu ya waathirika hao.
“iimeamua kwa dhati kuendelea kutoa msaada kwa waathirika ili kuweza kuwatibu wote waliopata majeraha kwenye kadhia hii ya bomu na kuwa wapo pamoja katika kila hali kuhakikisha wanapona kwa gharama yeyote”alisema Mulongo.
Wakati huo huo Viongozi wa kitaifa akiwemo Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wapo njiani kuja jijini hapa kuendelea kuwapa na kuwafariji wafiwa na waathirika wa bomu lililotupwa kwenye mkutano wa kampeni wa chama cha demokrasia na maendeleo(CHADEMA) wakati wakifunga kampeni ya uchaguzi mdogo wa udiwani kwenye kata ya Kaloleni jijini hapa juzi.