Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo amesimamisha kwa muda uchimbaji wa madini aina ya dhahabu katika machimbo ya Kitunda wilayani Sikonge ili kuepusha maafa zaidi yasije yakatokea.
Hatua hiyo inafuatia maafa yaliyokea hivi karibuni ambapo wachimbaji wadogo wadogo sita walifariki baada ya kufukiwa na kifusi na mmoja kufariki kwa kukosa hewa wakati wa uchimbaji wa dhahabu katika eneo la Kitunda wilayani Sikonge.
Uamuzi huo umetolewa jana wilayani Sikonge na Mkuu wa Mkoa wa Tabaora Bw, Mwanri baada ya yeye na kwa kushirikiana na Kamati na Ulinzi na Usalama mkoani humo kutembelea machimbo yalisababisha maafa hayo kwa ajili ya kujionea na kasha kuwapa pole wafiwa.
Alisema kuwa yeye na Kamati yake wameona ni vema wasimamishe kwa muda ili taratibu zote za kuhakikisha usalama na zile Baraza la Taifa la Mazingira za mpango wa ulinzi wa mazingira(Environmental Protection Plan) zinafuatwa kabla ya kendelea na shughuli za uchimbaji.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa lengo ni kutaka Wachimbaji hao waendele kuchimba katika hali ya usalama bila kuharatisha maisha yao na nguvu kazi ya Taifa.
Kufuatia hatua hiyo , Bw. Mwanri aliwaagiza Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kati na Magharibi Salim Salim na Afisa Madini Mkazi wa Tabora Laurent Mayala kuhakisha kuwa umbali kutoka shimo moja la uchimbaji hadi jingine unazingati matakwa ya Sheria na Kanuni kuliko ilivyo sasa ambapo kutoka shimo hadi shimo ni mita 3 hali ambayo ni hatari.