Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
MWENYEKITI wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo, amewahakikishia wananchi kuwa hali ya usalama wilaya ya Kibiti na Rufiji ipo shwari. Aidha amesema jeshi la polisi linaendelea na oparesheni mbalimbali za kuwasaka wahalifu wanaochafua mkoa na taifa.
Aliyasema hayo, kufuatia habari zinazoendelea kusemwa na kuandikwa katika baadhi ya vyombo vya habari kuhusu mambo yanayoendelea kwenye wilaya hizo. Mhandisi Ndikilo, aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa polisi waliopo kwenye oparesheni hiyo na kuacha kukimbia miji yao kama wanajiamini sio wahalifu.
"Kumekua na taarifa zinazoendelea kuandikwa suala ambalo mkoa haujawahi kutoa taarifa zaidi ya tukio la mauaji ya vifo nane iliyotokea april 13 na kukemea usafiri wa pikipiki ifikapo saa 12 jioni " alisema. Alibainisha kwamba, endapo kutakuwa na tukio ama jambo litakalojitokeza serikali ya mkoa, wilaya, jeshi la polisi litatolea ufafanuzi.
Mwenyekiti huyo wa kamati ya ulinzi na usalama ambae pia ni mkuu wa mkoa huo, alieleza, kuwa sasa vyombo vya dola vinawasaka watu waliojihusisha na mauaji ya wenyeviti wa vijiji, vitongoji na polisi . "Jeshi la polisi ama serikali haiwezi kumwonea mtu yoyote kwani inafanywa kwa kuzingatia sheria"alisema.
Mhandisi Ndikilo alisema jeshi la polisi linafanya kazi yake kwa weledi na kazi yake kubwa ni kulinda amani ya wananchi na mali zao. “Nawaombeni wananchi msiwe na hofu juu ya operesheni hiyo na hakuna haja ya kukimbia makazi yao kwani kuna taarifa kuwa kuna watu wamehama kwenye nyumba zao na kukimbia,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa watu wanaokimbia wanatia mashaka, hawana sababu ya kukimbia nyumba zao na familia zao kwani wanaotafutwa ni wahalifu na si raia wema. Mhandisi Ndikilo, alisema wananchi wanapaswa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili viweze kufanya kazi zake ipasavyo.
Aliwatoa hofu watu wote wanaofanya shughuli zao kwenye wilaya hizo kutokuwa na wasiwasi kwani ulinzi umeimarishwa .