Adhabu za viboko kwa watoto imeelezwa kuwa inachangia kwa kiasi kikubwa woga na kuwafanya washindwe kuwa wadadisi hali ambayo ina athari kubwa kwao kitaaluma.
Rais wa Rottary Club Mzizima, Ambroce Nshala alisema hayo juzi, wakati wa hafla ya chakula cha mchana na watoto waliolazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) iliyoandaliwa na Kituo cha Afrika Sana na Umoja wa makanisa hospitalini hapo.
Alisema Nshala kuwa ingawa serikali imerudisha adhabu hiyo lakini yeye binafsi anaona haipo sahihi kwani si lazima mtoto achapwe ndio aweze kujifunza kwani uzoefu unaonyesha kuwa viboko mara nyingi huwakanganya wanafunzi.
Alisema elimu bila viboko inawezekana kikubwa ni ushirikiano baina ya wazazi, walimu na walezi katika makuzi ya watoto na wale ambao inatokea wakakosea basi ni vema wakapewa adhabu mbadala kama vile kufanya usafi na hata kufagia.
“Watoto wapewe adhabu mbadala na sio viboko kwani aadhabu hizo zinaweza kuwajenga zaidi na kuwafanya watoto hao wakosefu kweli kujutia makosa yao badala ya kuwa kama ilivyo sasa” alisema na kuongeza kuwa adhabu ya viboko pia ina athari kisaikolojia kwa watoto.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Kituo cha Sanaa cha Afrika Sana Ailinda Sawe alisema watoto wa kike ambao ndio wengi kulingana na sensa ya hivi karibuni ndio wahanga wakubwa wa mambo yote yasiyofaa.
Alisema uamuzi wa kujumuika na watoto hao umetokana na taasisi yake na umoja wa makanisa hospitalini hapo kuguswa na kundi hilo la watoto ambao wengi wao wamelazwa hapo kwa muda mrefu kutokana na maradhi yanayowasumbua na amewataka wanajumuia wengine kulikumbuka kundi hilo.
“Kuna watoto hapa wamelazwa kwa miezi sita hadi mwaka na mbaya zaidi wengine wametoka mikoani na hawana ndugu wala jamaa hivyo wanahitaji msaada wa wanajamii” alisema na kuongeza kuwa watoto hao wanasumbuliwa na matatizo tofauti ikiwa ni pamoja na saratani ya damu, uvimbe wa vichwa na magonjwa mengine.
Rais wa Rottary Club Mzizima, Ambroce Nshala akizungumza wakati wa hafla hiyo chakula cha mchana.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sanaa cha Afrika Sana Ailinda Sawe pia alitoa neno wakati wa hafla hiyo.
Watoto wakitoa Burudani.