Na Karama Kenyunko, blogu ya jamii.
Mshtakiwa Philemon Manase ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa aliteswa sana wakati anatoa maelezo ya onyo katika kituo cha Polisi Osterbay Jijini Dar es salaam.
Ameyaeleza hayo leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi wakati akitoa utetezi wake katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi inayomkabili yeye, raia wa China anayedaiwa kuwa ni Malkia wa Pembe za Ndovu, Yang Feng Glan (66) na Silvius Matembo.
Akiongozwa na wakili wake, Nehemiah Nkoko, Manase amedai kuwa, alikamatwa Aprili 20, 2014 wakati akienda kununua vinywaji eneo la njia panda ya Segerea.
Amedai kuwa, baada ya kukamatwa, alipelekwa kituo cha polisi stakishali na baadae polisi osterbay ambapo wakiwa osterbay Sajenti Beatus aliagiza aandaliwe mazingira ya kumning'iniza kama popo na kwamba anataka amuhoji na taarifa zote wanazo.
Aliongeza kuwa polisi huyo alimwambia akikataa maelezo aliyokuwa nayo basi asije akamuomba msamaha kwa kitu ambacho wangemfanyia huku wakimuuliza kama alishawahi kukalia chupa.
Manase amedai alimuuliza mbona wanamtisha, lakini Beatus alichukua kalamu na karatasi na kuanza kuchukua maelezo yake binafsi.
Ameendelea kudai kuwa, wakati akihojiwa alimkabidhi afande Beatus simu mbili na Sh milioni 2.6 na kwamba kuna vijana wawili waliagizwa na afande huyo walikuwa na Bomba na wakamfunga pingu miguuni na bandeji mdomoni.
Aliendelea kudai kuwa walichukua hilo bomba wakamfunga miguu na mikono wakamuweka juu ya meza na kimning'iniza kichwa chini miguu juu. Akapigwa na rungu mara nne na kwamba alifanyiwa kitendo hicho kwa saa 3.
Baada alifunguliwa pingu za miguuni wakamuuliza kama yupo radhi kuendelea kutoa maelezo akamwambi ana hali mbaya anajisikia kizunguzungu na baadae afande Beatusi alimchukua nakumpeleka polisi Kijitonyama ambapo aliwekwa rumande.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 5, mwaka huu ambapo itatolewa uamuzi wa kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi kama kweli mshtakiwa huyo aliteswa wakati akitoa maelezo ya onyo ama la.
Kesi hiyo ndogo ndani ya kesi ya msingi imeanza kusikilizwa baada ya Wakili wa upande wa utetezi, Jeremiah Mtobesya kupinga maelezo ya onyo ya Manase yasipokelewe kama kielelezo cha kesi hiyo mahakamani kwa sababu aliyatoa polisi kwa sababu yalichukuliwa nje ya muda na alipigwa na kunyanyaswa.
Inadaiwa kuwa, kati ya Januari Mosi, 2000 na Mei 22,2014 kwa makusudi mshtakiwa Glan aliongoza na kufadhiri vitendo vya kijinai kwa kukusanya na kusafirisha vipande 706 vya Meno ya Tembo bila ya kuwa na kibali chochote kile kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyama Pori.
Ilidaiwa kuwa washtakiwa Salvius na Manase wanadaiwa kuongoza makosa ya uhujumu uchumi kwa kusaidia biashara ya nyara za serikali kwa kukusanya, Kusafirisha na Kuuza Meno ya Tembo kwa nia ya kujipatia faida.
Iliendelea kudaiwa kuwa Mei 21, 2014 katika eneo la Sinza Palestina wilaya ya Kinondoni mshtakiwa Manase alitoroka chini ya ulinzi halali wa askari wa Jeshi la Polisi D 7847 Koplo Beatus ambaye alikuwa akimshikilia kwa makosa ya kujihusisha na biashara za nyara za serikali.