Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii.
Fundi simu, Juma Maulid (30) mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, leo amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu tuhuma za kuingilia na kuchezea simu zilizofungiwa.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa imedaiwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali, Elizabeth Mkunde kuwa, mshtakiwa ametenda kosa hilo Novemba 8, 2016 katika maeneo ya Kariakoo mtaa wa Aggrey wilaya ya Ilala.
Mkunde amedai kuwa mshtakiwa huyo alighushi IMEI za simu aina ya Tecno L8 zenye namba 357085075221523 na 357085075221531 ambazo zilifungiwa na TCRA na kuzibadilisha namba hizo zikasomeka kama 352167055726443 na 352167055726450.
Mshtakiwa amekana kutenda kosa hilo na amerudishwa rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana. Hakimu Mwambapa alimtaka mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho watakaosaini hati ya dhamana ya maneno ya milioni tano kila mmoja.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 4 mwaka huu, kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali(PH) baada ya upande wa mashta kuileza mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika.
Akizungumza nje ya mahakama, Mwanasheria Mkuu Mwandamizi wa TCRA, Johannes Kalungula akiwa nje ya mahakama aliwaonya wale wote wanaojihusisha na kuingilia na kuchezea Imei za Simu zilizofungiwa ama kuibiwa watachukuliwa hatua za kisheria.
Ameongeza kuwa kitendo hicho kinarudisha nyuma zoezi lililofanyika la kufungia simu na kudhibiti wizi wa simu.