Na Veronica Simba – Dodoma.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo, amezindua Bodi mpya ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na kuiagiza kufanya kazi kwa kutanguliza maslahi ya Taifa na Watanzania kwa ujumla.
Profesa Muhongo alizindua Bodi hiyo jana, Aprili 19, 2017 Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma.
Akizungumza na Wakurugenzi wa Bodi hiyo mpya, wakati wa hafla ya uzinduzi, Profesa Muhongo aliwaagiza kuhakikisha wanawasimamia wakandarasi waliochaguliwa kutekeleza miradi ya umeme vijijini ili wanunue vitendea kazi ikiwemo nguzo, transfoma na nyaya za umeme kutoka kwa wazalishaji wa ndani ya nchi.
“Wakandarasi ni lazima wanunue vifaa hivyo ndani ya nchi. Vikiisha hapa nchini, ndiyo waagize nje. Hatutavumilia kuona mkandarasi ananunua vitendea kazi nje ya nchi wakati hapa nchini vipo tele.”
Hata hivyo, Profesa Muhongo alisisitiza suala la ubora ambapo alifafanua kuwa, ni lazima vitendea kazi vinavyonunuliwa viwe katika ubora unaostahili. “Japokuwa tunataka vitu kutoka ndani ya nchi lakini ni lazima tuzingatie suala la ubora wake.”
Akiendelea kutoa maagizo kwa Bodi hiyo, Waziri Muhongo pia alielekeza kwamba, Kampuni zote za kigeni ambazo zimeshinda Tenda ya kutekeleza miradi ya umeme vijijini awamu ya Tatu (REA III), ni lazima zifanye kazi na wakandarasi wadogo (sub-contractors) wa kitanzania.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe (kulia), akiwasomea majukumu yao ya kazi, Wakurugenzi wa Bodi mpya ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa Bodi hiyo, uliofanyika Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma, Aprili 19, 2017.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Bodi mpya ya REA, uliofanyika hivi karibuni mjini Dodoma.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa tano kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi wa Bodi mpya ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), mara baada ya kuizindua rasmi hivi karibuni mjini Dodoma. Kulia kwa Waziri ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara, Profesa James Mdoe na kushoto kwa Waziri ni Mwenyekiti wa Bodi, Dkt. Gideon Kaunda. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga..
KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA
KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA