Katika hotuba yake, Kaimu Balozi Spera aliieleza hafla hii kama sherehe ya kuthibitisha dhamira ya dhati ya wafanyakazi wa kujitolea kuhudumu na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani. “Serikali ya Marekani inafanya kazi katika maeneo yote – kuanzia utawala bora hadi maendeleo ya kiuchumi na usalama wa kikanda – lakini msingi wa kila tunachokifanya ni kuwasaidia watu wa Tanzania.
Tunafanya hivyo vyema zaidi pale panapokuwa na ushirikiano katika ngazi ya mtu na mtu. Dhamira hii hudhihirishwa kila siku na wafanyakazi wa kujitolea wa Peace Corps, wenyeji wao na wafanyakazi wenzao wa Kitanzania,” alisema Kaimu Balozi Spera.
Toka mwaka 1962, zaidi ya wafanyakazi wa kujitolea wa Peace Corps 2,850 wamehudumu nchini Tanzania. Peace Corps hutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa kujitolea wa Kimarekani wanaopangiwa kufanya kazi katika jamii wakihudumu katika nyanja za elimu ya sekondari (wakifundisha hisabati, sayansi na teknolojia ya Mawasiliano), afya na elimu ya mazingira.
Wafanyakazi wa kujitolea husaidia na kutoa mafunzo kuhusu utunzaji wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuzuia kuharibika kwa ardhi, kulinda vyanzo vya maji, kuhifadhi ardhi na matumizi ya mbinu bora za kilimo na uhifadhi wa misitu (agro-forestry) wakiweka msisitizo katika kufanya kazi kwa ubia na wanawake na vijana. Pia watatoa mafunzo na kuwezesha kuanzishwa kwa kilimo hai cha bustani (bio-intensive gardens) ili kuongeza upatikanaji wa chakula, na kuboresha lishe ya kaya pamoja na shughuli nyingine za kujiongezea kipato.
Aidha, wafanyakazi hawa wa kujitolea husaidia katika kuimarisha afya ya umma kwa kufanya kazi na vituo, vikundi vya kijamii na vile vilivyomo mashuleni vinavyotoa huduma na elimu ya afya ikiwa ni pamoja na zile zinazohusu kujikinga dhidi ya VVU/UKIMWI, matibabu na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU/UKIMWI,yatima na watoto walio katika mazingira hatarishi. Wafanyakazi wa kujitolea hufanya kazi kwa karibu na kamati za afya vijiji ili kubaini na kuchambua mahitaji na vipaumbele vya jamii na kushiriki katika shughuli zinazohamasisha mabadiliko ya tabia katika maeneo ya afya ya mama na mtoto, lishe, malaria, maradhi yanayosababishwa na maji yasiyo salama, afya ya uzazi na kinga dhidi ya VVU/UKIMWI.
Peace Corps ni taasisi ya Serikali ya Marekani iliyoanzishwa na Rais John F. Kennedy mwaka 1961 ambayo hivi sasa inahudumia zaidi ya wafanyakazi wa kujitolea zaidi ya 8,000 katika zaidi ya nchi 60 duniani. Kwa miaka 56, Peace Corps imekuwa taasisi inayoendesha shughuli za mabadilishano ya kiufundi na kitamaduni zisizoegemea mrengo wowote wa kisiasa na kidini. Zaidi ya wafanyakazi wa kujitolea 189,000 wamehudumu katika nchi 140.
Wafanyakazi wa kujitolea wa Kimarekani wa Peace Corps wapatao 51 wamekula kiapo cha utumishi wa miaka miwili nchini Tanzania katika hafla maalum iliyofanyika leo katika ofisi za Peace Corps jijini Dar es Salaam. Wafanyakazi hawa watakaohudumu katika sekta za afya na kilimo watapangiwa kufanya katika wilaya 20 nchini, ikiwa ni pamoja na wilaya za Iringa, Mufindi, Kondoa, Mbinga, Masasi, Ludewa, Lushoto, Songea, Kishapu, Makete na Singida vijijini. Wengine watapangiwa katika wilaya za Same, Njombe, Manyoni, Shinyanga vijijini, Mafinga, Makambako, Wanging’ombe, Mbeya na Lushoto.
Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Vincent Spera aliwaapisha wafanyakazi hao wapya wa kujitolea mbele ya mgeni rasmi, Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Huduma za Afya na Lishe katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dk. Athumani Amir Pembe, na Mkurugenzi Mkazi wa Peace Corps nchini Tanzania Dk. Nelson Cronyn.
Hafla hii ilihudhuriwa pia na waliowahi kuwa wafanyakazi wa kujitolea wa Peace Corps katika maeneo mbalimbali dunia, maafisa kutoka taasisi wabia na familia zilizowahifadhi wafanyakazi wapya wa kujitolea wakati wakiwa mafunzoni.