Na Stella Kalinga, Simiyu
Serikali mkoani Simiyu imeomba kuwepo kwa kikundi cha ulinzi cha kijeshi katika Wilaya ya Busega ili kusaidia mapambano dhidi ya vitendo vya uhalifu ikiwemo uvuvi haramu na kuwezesha ufugaji wa samaki ndani ya Ziwa Victoria kufanyika kwa usalama.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka wakati wa Hafla ya kumpongeza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi hapa nchini, Jenerali Venance Mabeyo iliyoandaliwa na ndugu zake kijijini kwao Yitimwila ‘A’ katika Kata ya Kiloleri Wilayani Busega.
“Tumepata changamoto nyingi sana kwenye ziwa, matukio mengi ya kihalifu liliwemo la uvuvi haramu , sisi kama mkoa tulikuja na wazo kwamba tungehitaji tupate ‘detouch’ moja eneo la Ziwa ili ukanda huu baada ya kufanya kazi kubwa ya kuchoma makokoro ya wananchi, tuwapeleke kwenye uvuvi wa kisasa hususani ufugaji wa samaki ziwani, jambo ambalo Mheshimiwa Rais analipa kipaumbele sana; na namna pekee ya kufanya ufugaji ule wa samaki ziwani, suala la ulinzi na usalama ni muhimu sana; ” alisema Mtaka.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo (katikati) akionesha siaha alizokabidhiwa na Wazee wa Busega kama ishara ya ushujaa kwake wakati wa hafla iliyoandaliwa na ndugu zake kijijini kwao Yitimwila A wilayani Busega kumpongeza kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.John Magufuli.
Aidha, Mtaka amesema pamoja na kufanya ufugaji wa samaki katika Ziwa Victoria, Serikali ya Mkoa imefanya makubaliano na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii NSSF kuwawezesha wananchi wa Busega kufanya kilimo cha Umwagiliaji kwa kutumia maji ya ziwa hilo ambayo ni ya uhakika.
“Tumeongea na NSSF kwa ajili ya kuanzisha mradi ambao hautazidi bilioni moja, tutaleta mbegu za aina ya nyanya na pilipili zinazotakiwa ili wananchi wa Busega wazalishe kwa wingi. Hatutakuwa tayari kuona wananchi wanalima nyanya na kuuza ndoo moja shilingi 500, tumepanga kuanzisha mradi wa kuzalisha ‘chill sauce’ na ‘tomato source’ .”alisema Mtaka.
Ameongeza kuwa Wataalam wa Wilaya na Mkoa kwa kushirikiana na Wataalam wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji , Kituo cha Utafiti wa Kilimo Ukiriguru wanafanya upembuzi yakinifu kuona namna miundombinu ya umwagiliaji itakavyojengwa ili kuwawezesha wananchi wa Busega kulima muda wote kupitia kilimo cha Umwagiliaji badala ya kutegemea mvua.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na viongozi na waalikwa katika hafla ya kumpongeza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Salvatory Mabeyo, kijijini kwao Yitimwila A wilayani Busega, kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.John Magufuli kwa nafasi hiyo.
Mtaka amesema Serikali mkoani Simiyu imedhamiria kuhakikisha katika kipindi cha miaka mitatu ijayo Mkoa hauingizi bidhaa kutoka mikoa mingine na badala yake wananchi wake watazalisha na kutumia bidhaa zao wenyewe, hivyo ameomba Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuona namna ya kuweka vituo vya kuuza zana za kilimo katika maeneo ya kanda ya Ziwa ili wananchi wapate zana bora za kisasa zitakazowasaidia kulima kisasa.
Kwa upande wake Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi hapa nchini, Jenerali Venance Mabeyo amewataka wananchi wa Busega kubadili mtazamo wao na kutumia maji ya ziwa Victoria kwa manufaa yao kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji ili wasikumbwe na tatizo la upungufu wa chakula kunapotokea ukame.