Na Benny Mwaipaja-Wizara ya Fedha na Mipango.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekutana na Taaasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) kwa lengo la kujadili namna ya kuboresha mazingira ya biashara nchini na kukuza uchumi ili kuiwezesha Tanzania kutimiza azma yake ya kuwa na uchumi wa viwanda.
Mkutano huo uliongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango (MB), Dkt. Philip Mpango pamoja na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji (MB), Mh. Charles Mwijage ulifanyika mkoani Dodoma katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango.
Katika mkutano huo Serikali ilipata nafasi ya kusikiliza baadhi ya changamoto ambazo zinaikabili Sekta hiyo na kuahidi kuandaa namna bora ya kuzitatua kwa manufaa ya Taifa.Akizungumza katika mkutano huo Dkt. Mpango alisema kuwa mkutano huo umelenga zaidi katika kuboresha mahusiano na uaminifu kati ya Sekta Binafsi nchini na Serikali.
“Sekta Binafsi na Sekta za Umma inabidi zifanyekazi kwa pamoja kwa maendeleo ya Taifa, niwaombe wafanyabiashara mtoe taarifa za watumishi wa Umma wasio waadilifu ili kuondoa hali ya kutoaminiana”, alisema.Dkt. Mpango aliongeza kuwa Serikali inaahidi kutatua kero mbalimbali zinazoikabili Sekta hiyo hususani suala la utitiri wa kodi na marejesho ya kodi ili kupunguza maumivu kwa wafanyabiashara na kukuza uchumi wa nchini.
Waziri wa Fedha na Mipango (MB), Dkt. Philip Mpango akisisitiza jambo mbele ya wadau wa Sekta Binafsi katika mkutano maalum wa Sekta hiyo na Serikali iliokuwa na malengo ya kuweka mazingira bora ya uhusiano na ushirikiano mwema katika kukuza uchumi wa nchi na kuiwezesha Tanzania kutimiza azma yake ya kuwa na uchumi wa viwanda ifikapo 2025.
Waziri wa Fedha na Mipango (MB), Dkt. Philip Mpango akimsikiliza mdau wa Sekta Binafsi, Bw. David Mwaibula kabla ya kupokea kitabu cha utafiti wa masuala ya Sekta hiyo, katika mkutano kati ya Serikali na Sekta Binafsi uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mjini Dodoma.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Dkt. Reginald Mengi akizungumza na wadau kutoka Serikalini na Sekta Binafsi ambapo ameiomba Serikali iwaamini wawekezaji wazawa kwa maendeleo ya Taifa na kuongeza kuwa Taifa lolote haliwezi kujengwa na wageni.
Baadhi ya viongozi mbalimbali wa Serikali wakifuatilia kwa makini maelezo ya wadau wa Sekta Binafsi wakati wa mkutano maalum wa Serikali na Sekta Binafsi uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mjini Dodoma.