BONANZA la Michezo la siku sita litakalohusisha walimu wa michezo na wadau mbalimbali linatarajiwa kufanyika Mei 20 mwaka huu kwenye viwanja vya Halmashauri ya Korogwe .
Bonanza hilo limefadhiliwa na asasi ya Inuka wenye lengo la kupiga vita madawa ya kulevya na kuhamasisha michezo na nidhamu kwa jamii
Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Mratibu wa Inuka Kanda ya Ziwa, Gaudance Msuya alisema lengo kubwa litakuwa kuiamsha jamii na kupenda kushiriki kwenye michezo ili kuimarisha afya zao.
Alisema katika bonanza hilo michezo itakayokuwepo ni mpira wa miguu,riadhaa ,mpira wa pete,kuvuta kamba na kukimbiza kuku na kutembea na magunia.
Aidha alisema washindi kwenye michezo hiyo wata zawadiwa zawadi mbalimbali ambapo zaidi ya milioni mbili zimetengwa kwa ajili ya zawadi kwa washiriki watakofanya vizuri.
“Ndugu zangu watu wa Korogwe hii ni fursa ya kipekee hivyo ninawaomba mjitokeze kwa wingi kushiriki kwenye bonanza hili ambalo litakuwa na faida kubwa licha ya kuwepo kwa zawadi hizo”Alisema.
Hata hivyo alisema kwa washiriki ambao wangependa kushiriki wawasiliane na Ofisa Michezo wilaya ya Korogwe ili kuweza kuthibitisha ushiriki wao.
Mratibu huyo aliyataka mashirika mbalimbali ikiwemo mabenki kuona namna ya kuunga mkono jambo hilo kwa kuona namna ya kufadhili ambapo wanaweza kuwasiliana na mratibu huyo kwa simu namna 0683122320/0683122340.