Na: Nuru Juma & Husna Saidi – MAELEZO
WATANZANIA waalikwa kushiriki katika mdahalo baina ya Diaspora na wenzao waishio nchini ili kujadili nafasi ya Diaspora katika uchumi wa nchi, unaotarajiwa kufanyika tarehe 11 na 12 April katika ukumbi wa Mzalendo Pub Jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa kampuni ya Ikolo Investiment Bw Maggid Mjengwa wakati akiongea na waandishi wa habari, leo jijini Dar es Salaam.
Mjengwa amesema kuwa Mdahalo huo umeandaliwa kwa lengo mahususi la kuwakutanisha kwa pamoja wadau wa maendeleo kwa ajili ya kusukuma mbele jitihada za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.
“Lengo la mdahalo huu ni kuwakutanisha watanzania waliopo Ughaibuni, watanzania waliokua wakiishi Ughaibuni na kwa sasa wamerudi na watanzania ambao hawakuwahi kufika Ughaibuni ili kuweza kujadili maendeleo ya nchi” alisema Mjengwa.
Aliongeza kuwa katika mdahalo huo pia utatumika kama sehemu ya maadhimisho ya miaka kumi ya kuanzishwa kwa mtandao wa Mjengwa Blog, mtandao ambao kimsingi ndiyo umekuwa daraja la kuwakutanisha Diaspora.
“Mdahalo huu ni pamoja na kuadhimisha miaka kumi ya Mjengwa Blog hivyo tumeona kuyafanya maadhimisho hayo kuwa ya tofauti kwa utofauti kuwajumuisha watanzania kujadili kwa pamoja mambo kadhaa kuhusu uchumi kwa lengo la kufanikisha maendeleo ya nchi kwa haraka zaidi.” Alisisitiza.
Nae Mratibu wa Vikoba Kimataifa Mwinyirwaka Hatibu alisema mdahalo huo pia utahusisha na mafunzo ya ujasiriamali kwa watanzania ili kuweza kufanikiwa kimaisha binafsi na kufanikiwa kwa taifa kiujumla.
“Katika kuhakikisha Tanzania inanufaika na Diaspora,yapata miaka mitatu sasa Serikali imekuwa ikiendesha mikutano kama hii kila mwezi wa nane kwa kuwaita watanzania waishio nje ya nchi kujadili uchumi na maendeleo ya nchi na kwa mara ya mwisho mkutano kama huu ulifanyika Zanzibar” alisema Hatibu.
Hata hivyo aliwasihi wanahabari na wananchi kwa ujumla kufika katika tukio hilo kwani watapata fursa ya kukutana na watu kutoka mataifa mbalimbali na kuweza kujifunza vitu vingi kutoka kwao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Ikolo Investment Ltd Bw. Maggid Mjengwa akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu mdahalo wa Diaspora kuhusu uchumi na maendeleo ya Taifa leo Jijini Dar es Salaam. Mdahalo huo utafanyika tarehe 11 mwezi April katika Ukumbi wa Mzalendo Pub uliopo Kijitonyama Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mratibu wa Vikoba Kimataifa Bw. Mwinyirwaka Hatibu.
Mratibu wa Vikoba Kimataifa Bw. Mwinyirwaka Hatibu akifafanua jambo na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu mdahalo wa Diaspora kuhusu uchumi na maendeleo ya Taifa leo Jijini Dar es Salaam. Mdahalo huo utafanyika tarehe 11 mwezi April katika Ukumbi wa Mzalendo Pub uliopo Kijitonyama Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Ikolo Investment Ltd Bw. Maggid Mjengwa.
Baadhi ya waandishi wa habari wakifatilia uongozi wa Ikolo Investiment LTD wakati wa mkutano wao na waandishi wa habari kuhusu mdahalo wa Diaspora leo jijini Dar es Salaam. Picha na Frank Shija– MAELEZO.