Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akifungua mkutano wa wadau wa nishati ulioambatana na uzinduzi wa Jukwaa la Nishati Tanzania (TEP) kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu jijini Dar es Salaam tarehe 05 Aprili, 2017. Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kujadili upatikanaji wa nishati endelevu ya kutosha kwa bei nafuu kwa ajili ya uchumi wa viwanda Tanzania.
Waziri wa Nishati na Madini,Profesa Sospeter Muhongo amesema nishati ya uhakika ya umeme itatokomeza umasikini nchini Tanzania ifikapo mwaka 2030. Profesa Muhongo aliyasema hayo alipokuwa akizindua Jukwaa la Nishati Tanzania (TEP) pamoja na mkutano wa siku mbili kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu mapema leo jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo unaolenga kujadili upatikanaji wa nishati endelevu ya kutosha kwa bei nafuu kwa ajili ya uchumi wa viwanda Tanzania, unakutanisha wadau mbalimbali zikiwemo kampuni za utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi nchini kama vile Statoil, BG na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Sehemu ya wadau wa nishati wakimsikiliza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani) katika mkutano huo.
Wadau wengine ni pamoja na kampuni za kuzalisha umeme kama vile Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Songas pamoja na mabalozi wa nchi mbalimbali, taasisi za kifedha na viongozi wa kiserikali.