Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa Tanzania ni Moja ya nchi salama kwa ajili ya uwekezaji barani Afrika kwa sababu haina matatizo ya migogoro ambayo yanaweza kuhatarisha usalama wa mali ya wawekezaji ikilinganishwa na nchi nyingine barani Afrika.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo wakati akifungua maonyesho ya Kibiashara kati ya Ufaransa na Tanzania yanayofanyika Jijini Dar es Salaam.
Makamu Rais Mhe Samia Suluhu Hassan pia amewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchini Ufaransa kuja kuwekeza katika maeneo mbalimbali hasa katika kilimo, nishati, utalii,usafiri kutokana na hali ya amani na utulivu iliyopo nchini.
Makamu wa Rais amesema maonyesho hayo ya kibiashara ambayo yataambatana na kongamano kubwa la Kibiashara kati ya nchi hizo Mbili ni fursa ya kipekee kwa wafanyabishara wa Tanzania na Ufaransa kukutana na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali ya kibiashara na uwekezaji.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Kongamano la kwanza la Biashara kati ya Ufaransa na Tanzania lililoandaliwa na Balozi wa Ufaransa nchini Bi. Malika BERAK (kulia), kushoto ni Mwenyekiti wa TPFS Dkt. Reginald Mengi.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Balozi wa Ufaransa nchini Bi. Malika BERAK kabla ya kukaribishwa kuhutubia hotuba ya ufunguzi wa Wiki ya Kongamano la kwanza la Biashara kati ya Ufaransa na Tanzania lililoandaliwa na Balozi wa Ufaransa nchini linalo fanyika jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiangalia moja ya picha ya majengo yaliosanifiwa na wataalamu wa majengo kutoka nchini Ufaransa kwenye maonyesho ya Bisahara kati ya Ufaransa na Tanzania lililoandaliwa na Balozi wa Ufaransa nchini.