Na Bashir Yakub
Transfer ni kubadilisha hati au leseni ya makazi kutoka jina la mmiliki wa awali kwenda kwa mmiliki mpya. Transfer inaweza kufanyika kutokana na mauzo, kupewa zawadi, fidia, n.k. Kwahiyo kuzuia transfer ni kuzuia kubadilishwa kwa hati kutoka mmiliki wa awali kwenda mmiliki mpya. Mara nyingi tumezoea kuzuia transfer kwa kutumia mahakama ( court injuction).
Sasa yatupasa tufahamu kuwa ipo njia nyingine nyepesi ambayo haihusishi mahakama. Ni njia ya maombi kwa kamishna wa ardhi kwa mujibu wa Sura ya 113 , sheria ya ardhi ,namba 4, ya mwaka 1999 vifungu vya 38, 39 na 41 . Kabla ya kuona ufanyeje kutumia njia hii ni vema tuone mazingira ambayo yakikutokea unaweza kutumia hiyo njia.
1.HAYA YAKITOKEA UNAWEZA KUPELEKA MAOMBI KWA KAMISHNA.
( a ) Mme wako au mke wako ameuza kiwanja au nyumba yenu na kuna namna ambavyo mauzo hayo unadhani sio halali kwasababu yoyote ile ya kisheria pengine ya kutokushirikishwa, au kushirikishwa lakini baadae kunyimwa haki yako kwa mujibu wa makubaliano au vinginevyo. Lakini wakati huo unadhani huna la kufanya kwakuwa mauzo tayari yamefanyika na pengine hata wewe ulishasaini.
( b ) Una maslahi na haki katika nyumba/kiwanja cha mirathi . Mali hiyo imeuzwa bila wewe kushirikishwa au umeshirikishwa lakini haki zako za msingi hazikuzingatiwa au namna nyingine yoyote ambayo kwayo unahisi mchakato haukwenda sawa. Lakini wakati huo unadhani huna la kufanya kwakuwa mauzo tayari yamefanyika na pengine hata wewe ulishasaini.
( c ) Umemuuzia mtu nyumba/kiwanja lakini amekataa kutekeleza baadhi ya makubaliano ya msingi yaliyo katika mkataba wenu wa mauziano na sasa anafanya mchakato wa kubadili hati.
( d ) Na mazingira mengine yoyote ambayo tayari nyumba/kiwanja kimeuzwa lakini ukaona kuna haja ya kuzuia mchakato wa kubadilishwa jina la mmiliki ili baadhi ya mambo yawekwe sawa kwanza.