BARAZA la Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), imeziteuwa timu ya Mamlaka ya Mapato Uganda (URA), Elect Sports ya Chad na Rayon Sports ya Rwanda kuziba nafasi ya timu za Tanzania zilizojitoa kwenye mashindano hayo yatakayoanza kutimua vumbi Juni 18 hadi Julai 2 Durfur nchini Sudan.
Mbali na timu hizo kuziba nafasi za timu za Tanzania pia baraza hilo linalazimika kupangua upya ratiba ya mashindano hayo na kupanga upya kesho kutwa Jumapili.
Katibu Mkuu wa Cecafa Nicholaus Musonye alisema wana timu nyingi hawawezi kubabaishwa na timu za Tanzania ambazo zimeshawishika na siasa na kuamua kujitoa katika mashindano hayo na kwamba maandalizi yote yamekamilika na mashindano yatafanyika kama yalivyopangwa.
"Tumeziteua timu hizo kwa vile tumejitaidi kuzishawishi timu tatu za Tanzania kushiriki michuano hii lakini zimegoma kwa kisingizio cha usalama licha ya kuwambia Sudani ni salama lakini hazijataka kutuamini.
"Mabadiliko ya ratiba yatafanyika wikiendi hii tutakapokutana mjini Khartoum na wajumbe wa Cecafa na waandaaji ambao ni viongozi wa Shirikisho la Soka la Sudan.
"Mashindano ni mazuri kwa ukanda wetu lakini siasa naona zimeingia kwenye soka na timu kujitoa bila ya sababu, hata hivyo mashindano yatafanyika kama kawaida, na maandalizi yanaendelea vizuri na serikali ya Sudan imeendelea kutusisitizia kutupa ulinzi wa hali ya juu.
Musonye alidai kuwa kitendo hicho ni sawa na hujuma huku akidai kuwa timu kubwa za El Merriekh na El Hilal zilijitoa kabla ya ratiba ya makundi kupangwa.Timu hizo zilijitoa kwa kuhofia hali ya usalama nchini Darfur na pia zikawa tayari kushiriki michuano hiyo kama ingefanyika Khartuom.
Hata hivyo Musonye alidai kuzichukulia hatua kali za kinidhamu timu zilizojitoa dakika za mwisho kwenye michuano hiyo wakati ratiba tayari imeshapangwa.
Timu zilizojitoa ni mabingwa watetezi wa michuano hiyo Yanga, Simba, Super Falcon ya Zanzibar na Tusker ya Kenya kutokana na hali duni ya usalama wa Darfur.
Timu hizo za Tanzania zimejitoa baada ya serikali kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje Benard Membe wakati akihitimisha hotuba ya bajeti ya wizara yake hivi karibun, alisema anashangaa kuona Sudan ikipewa uenyeji wa michuano hiyo licha ya kuwa na usalama mdogo na kuhoji busara iliyotumika kupeleka michuano hiyo huko.
Kauli hiyo ya Membe iliungwa mkono na msuluhishi wa mgogoro wa jimbo la Darfur nchini Sudan, Dk Salim Ahmed Salim ambaye alisema Sudan hamna usalama wa kuaminika licha ya vikundi kutokuwa na uadui na wachezaji na kutaadharisha kuwa vikundi hivyo vinaweza kufanya mashambulio kwa lengo la kufikisha ujumbe kama bado wapo na wanasilaha na kudai hakuna mantiki ya timu za Tanzania kushiriki michuano hiyo.
Hata hivyo jitihada za Mwenyekiti wa Cecafa Leodegar Tenga kutaka huruma ya serikali kuziruhusu timu za Tanzania kushiriki michuano hiyo ziligonga mwamba baaada ya juzi Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Amos Makalla kudai serikali haiwezi kuziruhusu timu za Simba, Yanga na Falcon kushiriki michuano hiyo kwa vile wana taarifa za kutosha kuwa Sudan Kusini hakuna usalama na nchi nyingine zimeendelea kujitoa, hivyo msimamo wao kama serikali, hawawezi kupeleka timu sehemu isiyo na usalama
Timu zitakazoshiriki michuano hiyo sasa ni Al Ahly Shandi (Sudan), Al Nasir (South Sudan), Al-Hilal Kadugli (Sudan), Express FC (Uganda), URA FC (Uganda), Ports FC (Djibouti), Vital’O (Burundi), Merriekh El Fasher (Sudan), APR (Rwanda), Elman (Somalia), Rayon Sport (Rwanda) Elect Sport (Chad) na Gor Mahia (Kenya).