Na Veronica Simba – Dodoma
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesaini leseni za madini kutoka kwa wawekezaji mbalimbali waliowasilisha maombi na kutimiza taratibu zote zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria.
Leseni ya kwanza iliyosainiwa ni ya uchimbaji wa kati wa dhahabu katika eneo la Masagalu, Handeni yenye namba ML 570/2016. Leseni hiyo imehamishwa kutoka kwa mmiliki wake wa awali ambaye ni Najim & Company Ltd kwenda kwa Shale Investments Tanzania Ltd.
Aidha, Waziri Muhongo alisaini leseni namba ML 572/2017 ya Sisti Mganga. Leseni hiyo ni ya uchimbaji wa kati wa madini ya ujenzi katika eneo la Itiso, Chamwino mkoani Dodoma.
Leseni nyingine iliyosainiwa na Waziri Muhongo ni ya uchimbaji wa kati wa madini ya ujenzi aina ya kokoto, ambayo mmiliki wake ni Said Abdallah. Leseni hiyo namba ML 573/2017 ipo eneo la Chipite, Masasi.
Profesa Muhongo aliwataka waombaji na wamiliki wote wa leseni za madini nchini, kuhakikisha wanatekeleza ipasavyo taratibu zote kama zilivyobainishwa katika Sheria ya Madini ikiwemo ulipaji wa mrabaha na kodi mbalimbali, kujenga mahusiano mema na jamii zinazowazunguka pamoja na kuzingatia utunzaji na uhifadhi wa mazingira.
Zoezi hilo la utiaji saini lilifanyika hivi karibuni, Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma na kushuhudiwa na wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Madini.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto), akisaini leseni za madini za wawekezaji mbalimbali waliowasilisha maombi na kukamilisha taratibu zote zinazotakiwa. Anayeshuhudia ni Mwanasheria wa Wizara, Khadija Ramadhan.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa pili kutoka kulia), akikabidhi leseni iliyohamishwa kutoka kwa mmiliki wake wa awali Najim & Company Ltd kwenda kwa Shale Investment Tanzania Ltd.