Na Bashir Yakub
Kutelekezwa ni pamoja na kunyimwa huduma za muhimu ambazo kama mke alistahili kupata. Huduma muhimu ni kama chakula, mavazi , makazi, matibabu, hela ya kujikimu kwa matumizi ya kawaida ya mwanamke, pamoja na kila hitaji ambalo kama mwanamke alitakiwa kulipata.
Ifahamike kuwa habari ya kutelekeza inawahusu wote mke na mme kwa maana ya kuwa mme anaweza kumtelekeza mke halikadhalika mke anaweza kumtelekeza mme. Hata hivyo makala yatazungumzia mme kumtelekeza mke ambapo sura ya 29 , Sheria ya ndoa iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 itarejewa.
1.AINA ZA KUTELEKEZA.
( a ) Aina ya kwanza ni kutelekeza ambako mume anaondoka kabisa ndani ya nyumba ambayo alikuwa akiishi na mke wake kama wanandoa na kwenda kuishi kwingine. Haijalishi huko alikoenda panajulikana ni wapi au hapajulikani suala la msingi ni kwamba hayupo katika makazi yake ya kawaida ya familia.
Aidha ikiwa hayupo nyumbani lakini kwa sababu za msingi na za kisheria huko sio kutelekeza. Sababu hizo ni kama kuwa jela, kuwa hospitali, kuwa amehamishiwa sehemu nyingine kwasababu ya matibabu kwa mfano wengine huamishiwa mikoani, na pia kuwa vitani labda baadae mkapoteza mawasiliano na mazingira mengine ya dharula za kibinadamu na ambayo siyo ya makusudi hayawezi kuitwa kutelekeza.
( b ) Aina nyngine ya kutelekeza ni hatua ya kuwa mme na mke wanaishi wote katika nyumba moja au chini ya paa moja lakini mume huyo hajishughulishi na kutoa matumizi au matunzo kwa mke huyo kwa namna yoyote ile. Hajui anakula nini, hajui anavaa nini, hajui anapata vipi matibabu, kwa ufupi hajui lolote zaidi ya kumuona tu kama binadamu wengine ambao anawaona mitaani na hana uhusiano nao.
Pia kuishi chini ya paa moja lakini vyumba tofauti nako ni kutelekeza hata kama mke anapewa matumizi yote yanayostahili. Zaidi, hata kulala chumba kimoja lakini vitanda tofauti kwa muda mrefu tena kwa makusudi kwasababu ya mgogoro wowote nako ni kutelekeza. Lakini pia kulala kitanda kimoja bila kushiriki tendo la ndoa kwa makusudi kwa muda mrefu bila sababu za msingi za kiafya au vinginevyo nako ni kutelekeza.