Aliyekuwa kocha Simba Patrick Liewig (pichani) amerejea nchini na kuitaka klabu hiyo imlipe malimbikizo ya mshahara wake kisha iachane naye kwa amani.
Simba iliachana na Liewig baada ya kutoridhishwa na matokeo ya mechi za msimu uliopita na kuishia kukamata nafasi tatu.
Akizungumza na Ripota wetu mara baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam jana alfajiri,Liewig alisema,hawezi kulazimisha Simba imwongezee mkataba isipokuwa anachohitaji ni malipo ya malimbikizo ya mishahara yake.
"Nimekuja hapa kwaajili ya kutaka kujua kinachoendelea, sababu nimesikia tu juu juu kuwa sitakiwi kwenye timu na sijaambiwa rasmi.
"Pamoja na hayo mimi sina tatizo,kama wameamua hivyo kuachana na mimi sawa isipokuwa wanilipe fedha zangu ninazodai kwani ni haki yangu na ndio maana nimekuja Tanzania"alisema Liewig
Aliongeza" Mkataba wangu umeisha Juni lakini kuna fedha zangu bado nawadai hivyo siwezi kuziacha hivi hivi, lazima wanilipe ndipo tumalizane kwa amani".
Kocha huyo aliichukua Simba mikononi mwa kocha aliyetimuliwa Milovan Cirkovic na alianza kuinoa timu hiyo kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kocha huyo alisifika kwa ukali wake kwa wachezaji na hivyo kuamua kufanya uamuzi mgumu wa kuwasimamisha baadhi ya wachezaji nyota wa timu hiyo kwa madai ya utovu wa nidhamu na kuwatumia vijana katika michezo 10.
Hata hivyo habari za ndani zinadai kuwa kocha huyo anaidai klabu hiyo malimbikizi ya mshahara wa miezi mitatu unaofikia kiasi cha dola 36,000.
Kaimu Makamu mwenyekiti wa Simba Joseph Itangare alisema hawana taarifa ya ujio wa kocha huyo lakini wanasubiri kama atawasiliana nao basi watamsikiliza.
"Sisi hatujui kama amefika hapa nchini lakini tunangoja kama atawasiliana na sisi tutafanya mazungumzo naye" alisema.