Maafisa Habari na Mawasiliano katika Wizara, Taasisi, Idara na Mamlaka za Mikoa na Wilaya nchini wametakiwa kutangaza mafanikio ya miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongoozwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli.
Hayo yamesemwa leo Mjini Morogoro na Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas wakati alipokuwa akizungumza na Maafisa Habari na Maafisa TEHAMA katika mafunzo ya uwekaji wa taarifa katika tovuti za Mikoa na Halmashauri yanayofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) na kusimamiwa na Ofisi ya Rais- TAMISEMI na Wakala ya Serikali Mtandao (EGA).
Kwa mujibu wa Dkt. Abbas alisema Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika Mikoa na Halmashauri zake, hivyo ni wajibu wa Maafisa Habari kuhakikisha kuwa taarifa zinazowekwa katika tovuti hizo zinaonyesha mafanikio ya Serikali katika utekelezaji wa miradi hiyo.
“Ipo miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ikiwemo miradi ya umeme vijiji, ambapo Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi hiyo, hivyo ni wajibu wa Maafisa Habari kuhakikisha kuwa taarifa za utekelezaji wa miradi inawafikia wananchi” alisema Dkt. Abbas.
Aliongeza kuwa lengo la Serikali ya Awamu ya Tano inayooongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magaufuli ni kuleta matokeo ya haraka kwa wananchi wake, hivyo ni wajibu wa Maafisa Habari kuhakikisha taarifa mbalimbali za mafaniko katika maeneo yao ya kazi zinatangazwa kwa kuzingatia muda na wakati.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas akizungumza na Maafisa Habari na Maafisa TEHAMA katika mafunzo ya uwekaji wa taarifa katika tovuti za Mikoa na Halmashauri yanayofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) na kusimamiwa na Ofisi ya Rais- TAMISEMI na Wakala ya Serikali Mtandao (EGA). Kwa taarifa kamili BOFYA HAPA