NA MAGRETH KINABO- MAELEZO
BARAZA la Uuguzi na Ukunga Tanzania limetoa agizo kwa mtu, kikundi au taasisi inayoendesha mafunzo ya uuguzi na ukunga bila kuwa na kibali kufunga mara moja.
Aidha baraza hilo limewataka wamiliki wa vyuo hivyo, wafuate taratibu zinazotakiwa ili kuhakikisha vyuo vyao vinasajiliwa.
Kauli hiyo imetolewa leo na Msajili wa vyuo hivyo kutoka katika baraza hilo, Lena Mfalila wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari- MAELEZO jijini Dares Salaam.
Alisema baraza hilo ,linafanya kazi chini ya sheria inayoitwa ‘The Nursing and Midwifery Act’ ya mwaka 2010 namba 1 ili kuhakikisha kuwa huduma za afya inayotolewa kwa umma ni bora na salama.
“Kuanzia sasa baraza halitasita kuchukua hatua za kisheria kwa wle wote watakaokiuka agizo hili, ni vyema tukazingatia wito wa kutii sheria bila shuruti,” alisema Mfalila.
Aliongeza kuwa kuanzisha mafunzo ya uuguzi bila kibali cha mamlaka husika, ambayo ni baraza hilo ni uvunjaji wa sheria. Hivyo katika sheria ya baraza hilo kifungu namba 41 kinaeleza hatua zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya mtu,taasisi,kikundi chochote kitakachokiuka sheria hii.
Akifafanua kuhusu kifungu hicho, Afisa Muuguzi Mkuu –Kitengo cha Mipango na Fedha alisema , Andrew Kapaya alisema sheria iko wazi kifungu cha 41 sehemu ya nane inatoa adhabu kwa mtu atakayekiuka kuwa atatoa faini ya sh.milioni tatu au sh. milioni tano au kifungo cha miaka mitano au vyote kwa pamoja.
Hata hivyo Mfalila alisema wana mpango wa kuanzisha utaratibu mpya wa kufanya kazi kwa pamoja yaani wataalamu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wa kitengo hicho, baraza hilo na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) ili kuhakikisha vyuo vya taalauma hivyo vimekidhi masharti ya usajili.
Baraza hilo limewataka wananchi kuacha kuandikisha vijana wao katika vyuo ambavyo vinaendesha mafunzo kinyume na utarati bu kwa kuwa wale wote wanaohitimu katika vyuo hivyo hawatambuliwa na baraza hilo na hawatasajiliwa kama wauuguzi wa wakunga hapa nchini na duniani kote.