SIKU moja baada ya Simba kumalizana na mchezaji wake Amri Kiemba (pichani), mchezaji huyo sasa yupo sokoni na atauzwa kwenye timu ya Wydad Casablanca ya Morocco. Kiemba alimwaga wino wa kuichezea Simba kwa miaka miwili jana kwa dau la Sh35 milioni huku atakuwa akikunja mfukoni kitita cha Sh2 milioni kama mshara wake.
Awali mchezaji huyo alikuwa akiwaniwa na mahasimu wao Yanga, na Simba ingezubaa basi kiungo huyo angerejea nyumbani kwa mabingwa hao wa Tanzania bara. Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Zakaria Hanspope tayari ametua Morocco akitokea Tunisia ambako alikwenda kufatilia fedha zao za usajili wa mshambuliaji wao Emanuel Okwi anayekipiga kweney timu ya Etoile du Sahel nchini Tunisia.
Okwi alijiunga na timu hiyo ya Tunisia mapema mwaka huu baada ya Simba kumuuza kwa dola 300,000 lakini klabu hiyo ya Etoile Du Sahel imekuwa ikizingua kulipa fedha hizo.
Lakini jana Hanspope alisema "Nimeshatoka Tunisia nipo Moroco na nimeshafanya mazungumzo ya awali na viongozi wa Wydad Casablanca n kesho tunafanya mazungumzo ya mwisho kabla sijarejea Dar, kila kitu kinaenda vizuri, naamini tutafikia mwisho mzuri."
Simba waliingia mchecheto wa kumsajili mchezaji huyo baada ya kutonywa na kigogo mmoja wa TFF ambaye pia ni mnazi mkubwa wa Simba kuhusu timu hiyo kuvutiwa na Kiemba na kushauri asajiliwe haraka ili Simba wapate faida kwa kumuuza.
Casablanca walimuona mchezaji huyo wakati wa mchezo kati ya Stars na Morocco ambapo Stars ililala kwa mabao 2-1 goli ambalo la ni kufutia machozi lilifungwa na Kiemba.