Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
Timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 Serengeti Boys imepangwa Kundi B katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17, zitakazofanyika nchini Gabon kuanzia Mei 14 hadi 28, mwaka huu.
Serengeti walifuzu kuingia katika fainali hizo baada ya kushinda rufaa yao dhidi ya Congo Brazaville kushindwa kumpeleka mchezaji wao aliyechezeshwa kwenye kikosi cha vijana lakini akisadikiwa kuwa ni mkubwa kiumri tofauti na kanuni za mashindano hayo.
Congo Brazaville walishindwa kumuwasilisha kwa vipimo zaidi ya mara tatu walipohitajiwa na CAF na hivyo CAF kuamua kuwaondoa kwenye nafasi hiyo na kuchukuliwa na Tanzania..
Kundi B, Serengeti Boys wamepangwa na Angola, Niger na Mali ambapo kwa sasa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) limewafungia baada ya Serikali ya nchi hiyo kuingilia masuala ya soka na kuwafukuza viongozi wa Shirikisho la Soka la nchi hiyo (FEMAFOOT).
Kundi A lina timu za wenyeji Gabon, Guinea, Cameroon na Ghana na ikumbukwe timu mbili za juu kila kundi zitafuzu moja kwa moja Fainali za Kombe la Dunia za U-17 nchini India baadaye mwaka huu.
Awali fainali hizo zilitakuwa kufanyika nchini Madagascar lakini Gabon aliyekuwa rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Issa Hayatou wa Cameroon alisema nchi hiyo haikukidhi vigezo vya kuandaa mashindano hayo.

Kikosi cha timu ya Tifa ya vijana chini ya miaka 17 Serengeti Boys.