Raia sita wa Pakistani na mmoja wa Sri-Lanka wanaoishi jijini Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakamani wakikabiliwa na mashitaka saba likiwemo la kula njama, kutoa huduma ya mawasiliano ya kimataifa bila kibali cha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kuisabishia serikali na mamlaka hiyo hasara ya Sh. Milioni 459.
Washtakiwa hao wamesomewa mashitaka yao leo mbele ya Hakimu Mkazi Wilbard Mashauri wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam. Jamhuri imewakilishwa na Mawakili wa Serikali Nassoro Katuga aliyekuwa akisaidiana na Mwanasheria Mkuu wa TCRA, Johannes Karungula.
Wakili Katuga amewataja watuhumiwa hao kuwa ni, Dilshad Ahmed,Rohail Yaqoob, Khalid Mahmood, Ashfaq Ahmad, Muhammad Aneess, Ramesh Kandasamy na Imtiaz Ahamad Ammar.
Katika shtaka la kwanza imedaiwa, kabla ya Novemba mwaka Jana, jijini Dar es Salaam, washtakiwa walikula njama ya kutenda kosa la matumizi ya Huduma za network kinyume cha sheria.
Katika shtaka la pili, washtakiwa hao wamedaiwa, kati ya Novemba mwaka Jana na Februari mwaka huu, bila halali na kwa makusudi washtakiwa wakiwa na nia ya kukwepa malipo halali walitoa huduma ya mawasiliano ya kimataifa bila leseni ya TCRA.