Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii
Kikosi cha Yanga kimeendelea na mazoezi yake leo kwenye Uwanja wa Taifa ikiwa ni maandalizi ya kuelekea mechi ya marudiano ya michuano ya klabu Bingwa Afrika dhidi ya Zanaco utakaofanyika mwishoni mwa wiki hii.
Mechi hiyo inayotarajiwa kuwa Jumamosi Machi 18, itachezwa Nchini Zambia ambapo katika mchezo wa awali timu hizo zilitoka sare ya 1-1.
Akizungumza na mtandao huu, Meneja wa Yanga Hafidh Saleh amesema kuwa kikosi kinaendelea na mazoezi ya kujiandaa na mchezo huo wa marudiano utakaofanyika nchini Zambia huku washambuliaji wawili wa kimataifa wakiwa hawajajiunga na wenzao.
Saleh amesema, Amisi Tambwe na Donald Ngoma bado wapo katika uangalizi wa daktari na hawajajiunga na wenzao katika mazoezi kuelekea mechi ya marudiano.
"Kwa sasa tunaendelea na mazoezi hapa Uwanja wa Taifa, Tambwe na Ngoma wakiwa hawajajiunga na wenzao kwani bado wapo chini ya uangalizi wa daktari, wachezaji wengine wote wapo fiti wakiendelea kujifua" amesema Saleh.
Kesho kocha Mkuu wa Yanga George Lwandamina anatarajia kutaja kikosi kitakachoondoka siku ya Alhamis kuelekea nchini Zambia kwa ajili ya marudiano na Zanaco na Yanga inahitajika kupata ushindi wa goli 1-0 ili iweze kusonga mbele kwenye hatua ya makundi ya klabu Bingwa Afrika.