Kamati za Kudumu za Bunge zitaanza kukutana Mjini Dodoma kutekeleza majukumu yake kuanzia Tarehe 20 Machi, 2017 hadi Tarehe 2 Aprili, 2017 kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Saba wa Bunge uliopangwa kuanza Tarehe 4 Aprili 2017. Kufuatia shughuli hizi za Kamati, Waheshimiwa Wabunge wanatarajiwa kufika Mjini Dodoma Jumapili tarehe 19 Machi, 2017.
Pamoja na Shughuli nyingine zitakazotekelezwa na Kamati katika Kipindi hiki, kuanzia Tarehe 20 hadi 27 Machi 2017, Kamati zitatembelea maeneo mbalimbali nchini kukagua miradi ya maendeleo iliyotengewa fedha kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 inayotekelezwa na Wizara/Idara zinazosimamiwa na Kamati husika.
Baada ya ziara hizo kukamilika, Kamati zitachambua Taarifa za utekelezaji wa Bajeti za Wizara inazozisimamia kwa Mwaka wa Fedha unaoisha kwa ajili ya kufanya ulinganisho kuhusu makadirio ya matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha unaofuata.
Aidha, kulingana na matakwa ya kikanuni, Tarehe 28 Machi, 2017 kutakuwa na Mkutano wa Wabunge wote kwa ajili ya kupokea Mapendekezo ya Serikali kuhusu Mpango na Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
Ratiba zote za Shughuli za Kamati za Bunge ikiwa ni pamoja na maeneo ambayo kamati hizo zitafanya ziara, vinapatikana katika Tovuti ya Bunge ambayo ni www.parliament.go.tz.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano
Ofisi ya Bunge
DODOMA