Na Bashir Yakub.
Mara nyingi wazazi wanapotengana huwa tunashuhudia mabishano ya nani anatakiwa kukaa na mtoto. Ni mama au baba. Kwa suala hilihili wapo watu wako mahakamani na wengine hawako mahakamani lakini wako katika ugomvi mkubwa wa nani haswa akae na mtoto.
Wapo ambao walikuwa katika ndoa na sasa ndoa imevunjika, wapo ambao walikuwa wakiishi kama mke na mme lakini bila ndoa na sasa mahusiano yao yamekwisha na wapo ambao hawakuwahi kufunga ndoa wala kuishi kama mke na mme ila walizaa tu ila kwasasa wapo katika mgogoro wa nani akae na mtoto.
Makala yataeleza namna sheria inavyozungumza kuhusu umri wa mama kukaa na mtoto lakini kabla ya hilo ni vema pia kutizama ni wapi waweza kupeleka malalamiko ya jambo hili. Sheria ya Mtoto , namba 21 ya mwaka 2009 ndiyo inayohusika katika jambo hili.
1.WAPI UKALALAMIKE UKITAKA KUKAA NA MTOTO.
Zipo sehemu mbili ambazo waweza kupeleka malakamiko yako ili uweze kupatiwa haki ya kukaa na mtoto. Kwanza ni ustawi wa jamiii na pili ni mahakamani.
Mahakama yoyote ya mwanzo, wilaya, hakimu mkazi hata mahakama kuu unaweza kupeleka mombi haya. Ila ni vema ukaanza mahakama ya mwanzo au wilaya.
Tofauti ya ustawi wa jamii na mahakamani ni kuwa mahakama wana amri wakati ustawi wa jamii hawana amri( order) .