Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameutaka uongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) kushiriki kikamilifu shughuli za matengenezo ya vivuko ili kupata ujuzi wa ufungaji wa mifumo kutoka Kampuni zinazotengeneza vivuko vya Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kivuko kipya cha MV Kazi, Bandarini jijini Dar es Salaam, Waziri Prof. Mbarawa amesema kuwa kupitia mafunzo hayo Serikali itaweza kuokoa fedha nyingi ambazo kwa sasa inatumia kulipa kampuni binafsi zinazojenga na kukarabati vivuko
“Hakikisheni mnapata ujuzi kama walionao hawa, hatutaki kutumia fedha za Serikali kwa ajili ya kukarabati au kutengeneza vivuko wakati nyinyi TEMESA mpo”, amesema Waziri Prof. Mbarawa
Pamoja na ujenzi wa kivuko hicho Waziri Mbarawa amewataka Temesa kuhakikisha wanasimamia na kukitunza kivuko hicho ili kiweze kudumu kwa muda mrefu.
Aidha, Profesa Mbarawa ameuagiza Wakala huo kuhakikisha wanakamilisha mifumo ya ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki ili ili kudhibiti mianya ya rushwa.
Kuhusu huduma za kivuko mkoani Lindi Serikali imesema itahakikisha inapelekea huduma haraka iwezekanavyo ili kurahisisha usafiri kwa wananchi wa mkoa huo.

Kivuko cha MV. Kazi kikiwa katika hatua za mwisho za ujenzi wake.Kiuvko hicho kitakamilika na kuanza tarehe 15 mwezi huu na kina uwezo wa kubeba abiria 800 na magari 22 kwa wakati mmoja.

Meneja Mradi wa Kampuni ya Songoro Marine Transport inayojenga Kiuvko cha MV. Kazi, Bw. Major Songoro, akitoa ufafanuzi wa mashine kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, alipokagua Kivuko hicho jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (kulia), akiangalia moja ya vifaa vilivyoko kwenye chumba cha kuendeshea kivuko katika kivuko cha MV. Kazi kinachojengwa jijini Dar es Salaam. Kivuko hicho kitakabidhiwa tarehe 15 Mwezi huu. Wa pili kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA), Dkt. Musa Mgwatu.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (kulia), akifafanua jambo kwa Uongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA), mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kivuko kipya cha MV Kazi ambacho kinatengenezwa jijini Dar es salaam na Kampuni ya Songoro Marine Transport.