Na Bashir Yakub
1.KUNYIMWA MTOTO.
Wako watu ni wazazi na wamezaa lakini wameyimwa watoto. Zipo sababu nyingi zinazopelekea hili. Matukio ya namna hii hayawatokei sana wanawake na badala yake wanaume ndio waathirika zaidi katika hili . Ni rahisi na kawaida mno mwanaume kuambiwa na mzazi mwenzake kuwa huyu mtoto si wako hata kama anajua kabisa huyo mwanaume ndiye mzazi halisi . Leo haya sio maajabu tena.
Upo usemi wao kuwa mwanamke ndiye anayejua baba wa mtoto. Sitaki kueleza ukweli au upotoshi wa usemi huu bali nawaza iwapo ni sawa kutumia usemi huu kupora haki ya uzazi wa mtu ambaye unajua kabisa ndiye mzazi halisi.
Na kwa bahati mbaya wanaokutwa na kadhia hii wamekuwa hawajui ni hatua zipi wachukue. Wapo wanaoamua kufanya vurugu, wapo wanaojiua, wapo wanaoamua kumuachia mola, na wengine hukimbilia serikali za mitaa ikiwa ni pamoja na hatua nyinginezo zisizofaa.
Ukweli ni kuwa hatua hizo haziwezi kukusaidia zaidi utapoteza muda mwingi, gharama na pengine kuzua matatizo mengine ambayo hayakuwako.
Basi sasa yafaa ujue kuwa sheria imetambua jambo hili na imeweka taratibu nzuri za kufuata ili kuondoa ujeuri wa aina hii.
Sheria Namba 21, Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 imeeleza nini ufanye kama tutakavyoona hapa chini. Lakini kabla ya hilo hebu kwa kutaja tu tuone sababu kadhaa zinazofanya wazazi hasa wa kike kuwanyima wazazi wenzao haki ya kutambulika kama wazazi wenzao.