Na Bazil Makungu Ludewa
MAHAKAMA ya Wilaya ya Ludewa katika Mkoa wa Njombe imemhukumu kwenda jela miezi kumi na mbili na kunywang’anywa leseni ya udereva na kisha kufungiwa kutoendesha gari lolote katika maisha yake Edward Mliwa kwa kusababisha majeraha kwa watu watano baada ya kupata ajali kwa uzembe.
Akisoma hukumu hiyo iliyochukua takribani masaa mawili hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Ludewa Fredrick Lukuna alisema kuwa mahakama yake imeridhika na ushahidi ulioletwa mbele yake na upande wa mashtaka na kwamba mshtakiwa atatumikia kifungo cha miezi kumi na mbili jela au kulipa faini ya sh hamsini elfu (50,000) kwa kila kosa.
Lukuna mshtakiwa Edward Mliwa anashtakiwa kwa makosa matano ikiwemo kuendesha chombo cha moto kwenye barabara ya umma kwa uzembe na kusababisha ajali iliyowajeruhi watu watano kinyume na sheria chini ya kifungu 41, 50 na 63(2) cha sheria barabarani sura ya 168.
Hakimu mkazi mfawidhi akaendelea kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Novemba 12 mwaka 2012 katika kijiji cha Masasi barabara ya Ludewa Manda wilayani Ludewa ambapo alikuwa akiendesha gari aina ya center yenye namba za usajiri T 715 AZU akiwa amebeba abiria kupita kiasi.
Awali mshtakiwa alikiri kosa moja tu ambalo ni kusababisha majeraha kwa abiria watano lakini akakana kuhusika na kosa na uzembe akiwa na chombo cha moto hata hivyo mahakama hiyo imeiamuru mamlaka ya mapato nchini TRA kuifungia leseni ya mshtakiwa maisha kutokana na makosa hayo.
Akiomboleza mahakani hapo Edward Mliwa akaiomba mahakama kumwonea huruma na kumpunguzia adhabu kwa sababu anayofamilia inayomtegemea, hata hivyo alilipa faini na kupona kwenda jela.