FAINALI za Taifa za michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 za Airtel Rising Stars zimepangwa kuanza kutimua vumbi uwanja wa Kumbu Kumbu ya Karume jijini Dar es Salaam Julai 2 kwa mabingwa watetezi Temeke wavulana kupambana na Kinondoni.
Akizungumza wakati wa semina elekezi ya Airtel Rising Stars 2013 iliyofanyika Juni mosi katika ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Ofisa Maendeleo wa shirikisho hilo Bw. Salum Madadi alisema ARS ngazi ya mikoa imepangwa kuanza Juni 15 hadi 29.
Mikoa inayoshiriki Airtel Rising Stars mwaka huu kwa upande wa wavulana ni mikoa ya kisoka ya Ilala, Kinondoni na Temeke. Mikoa mingine ni Morogoro Mwanza na Mbeya ambapo kila mkoa unatakiwa kushirikisha timu sita.
Usajili wa timu umepangwa kuanza rasmi kesho Juni 2 na kumalizika Juni 11. Kwa upande wa timu za wasichana, alisema, mikoa itakayoshiriki ni Tanga, Kigoma na Ruvuma na mikoa yote inayoshiriki Airtel Rising Stars mwaka huu iliwakilishwa kwenye semina elekezi na makatibu wakuu ambao walipata fursa ya kupitia kanuni na taratibu za michuano hiyo ya vijana.
Upangaji wa ratiba uliofanyika leo ni wa fainali za taifa pekee kwa kuwa mashindano ya ngazi ya mkoa yataendeshwa na uongozi wa mkoa husika ikiwa ni pamoja na kupanga ratiba yake.
Kwa upande wa wasichana timu zitakazofungua dimba katika fainali za taifa ni Ilala na Kinondoni. Kwa ujumla timu 12 zitashiriki fainali za Taifa, sita za wasichana na sita za wavulana.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo, Meneja wa Uhusiano wa Airtel Tanzania, Jackson Mbando alitoa rai kwa makatibu wakuu wa mikoa kuwa makini wakati wa usajili ili kupata vijana wenye vipaji ambao wataiwakilisha vema Tanzania kwenye michuanoa ya kimataifa ya Airtel Rising Stars.
Vile vile Tanzania itawakilishwa kwenye klini itakayofanyika chini ya makocha wa Manchester United. Alisisitiza alisema nia thabiti ya Airtel Tanzania kuendelea kusaidia mashindano ya vijana kwa nia ya kuendeleza soka nchini na kuishukuru TFF na wizara inayohusika na michezo kwa kuyaunga mkono mashindano haya.
Naye mgeni rasmi katika semina hiyo , Katibu Mkuu wa Chama Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Msafiri Kondo aliwaomba wadhamini kuendelea kudhamini michuano hiyo ili vijana wa kike na kiume waweze kufikia malengo yao katika soka. Mwisho….
Baadhi ya makatibu wakuu wa mikoa wa vyama vya soka vya mikoa inayoshiriki michuano ya soka ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars wakifuatilia kwa makini kanuni za mashindano hayo wakati wa semina elekezi iliyofanyika TFF leo.
Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania Bw. Jackson Mmbando akiongea na makatibu wakuu wa mikoa na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa semina elekezi ya Airtel Rising Stars iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa TFF leo.
Katibu mkuu mkoa wa kisoka wa Temeke Mbarouk Mhamed (kulia) akichukua karatasi wakati wa kupanga makundi na ratiba ya michuano ya Taifa ya Airtel Rising Stars iliyopangwa kuanza mwezi Julai, 2013 uwanja wa Kumbu Kumbu ya Karume jijini Dar es Salaam. Kushoto ni katibu wa DRFA Msafiri Kondo.