Na Abdulaziz Video,Lindi
Jeshi la Polisi Mkoani Lindi linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kusambaza taarifa za kupotosha wananchi zenye viashiria vya uchochezi na vitisho kwa serikali kwa lengo la kuvuruga amani, upendo na utulivu wa wananchi.
Akitoa taarifa kwa wandishi wa habari, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi George Mwakajinga amesema watuhumiwa hao wamekutwa wakiwa na mabango yenye maandishi ya uchochezi kwa watu wa mikoa ya Kusini.
Amesema kati ya watuhumiwa hao wawili, mmoja anatambuliwa kwa jina la Ivon Vandu Taasa mkazi wa Sabasaba ktk Manispaa ya Lindi ambaye alikutwa eneo la kituo cha mabasi ktk Manispaa hiyo akihamasisha wananchi kuunga mkono vurugu zinazofanywa na wananchi wa Mkoa wa Mtwara akiwa akiwa na mabango ya karatasi yenye maneno "Gesi kwanza Uhai baadaye".
Kwa mujibu wa Kamanda huyo wa Polisi, mtuhumiwa mwingine ambaye jina lake linahifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi, anatuhumiwa kusambaza ujumbe wa simu kwa watu mbali mbali zenye kuchochea na kutoa vitisho dhidi ya serikali na jamii na katika tukio lingine Mkazi wa kijiji cha Majengo wilaya ya Nachingwea Mkoani Lindi Silvanus Patrick, anashikiliwa na jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa kidato cha pili ktk shule ya sekondari Msufini wilayani humo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi George Mwakajinga amesema kuwa mtuhumiwa huyo anadaiwa kufanya kosa hilo usiku wakati mwanafunzi huyo akitokea dukani alikotumwa na wazazi wake kununua mafuta ya taa kwa matumizi ya nyumbani kwao.
Mwakajinga amesema baada ya mwanafunzi huyo kudai kufanyiwa kitendo hicho, aliwaarifu wazazi wake ambao walitoa taarifa kituo cha Polisi wilaya ya Nachingwea na kufanikiwa kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo.
Mwakajinga amesema kutokana na kitendo hicho, mwanafunzi huyo alipelekwa hospitali ya wilaya ya Nachingwea kwa uchunguzi wa kitaalamu na kubainika kufanyiwa kitendo hicho na kwamba mtuhumiwa anatazamiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya polisi kukamilisha taratibu zote za kisheria.