Na Mashaka Mhando, Korogwe
KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mustapha Jaffer Sabodo ameipatia wilaya ya Korogwe visima vitatu vitakavyogharimu kiasi cha shilingi milioni 60 ambavyo vitachimbwa katika maeneo ya Korogwe Mjini na Korogwe Vijijini.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Korogwe juzi Sabodo ambaye hadi kufikia jana tayari amechimba visima 245 katika maeneo mbalimbali nchini, atachimba visima hivyo kupitia taasisi yake mpya ya Sabodo Water Wells Faundition inayoongozwa na mwenyekiti wake Profesa Mark Mwandosya.
Alisema ameamua kuisadia wilaya ya Korogwe kutokana na adhima yake aliyoiweka ya kusaidia jamii ya Watanzania nchini kutokana na suala la maji kuwa kero katika maeneo mengi hivyo kusaidiana na serikali katika kutatua kero hiyo.
"Nitatoa visima vitatu viwili katika jimbo la Profesa Majimarefu na kimoja nimepa Mama mary Chatanda Korogwe mjini, lakini vingine 15 nitawachimbia mwenzi Desemba mwaka huu, vitano Korogwe mjini na kumi korogwe vijijini," alisema Sabodo.
Akizungumza katika eneo la Kwasemangube ambalo litachimbwa kisima kimoja, Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani 'almaarufu Profesa Majimarefu, alimshukuru Sabodo kwa msaada wake wa kusaidia visima hivyo ambavyo vitaondopa kero ya maji katika maeneo ambayo vitachimbwa.
Alisema katika visima viwili atakavyowapa Sabodo, kimoja kitachimbwa katika Kijiji cha Magamba kwalukonge na kingine kitachimbwa katika kijiji cha Kijango kilichopo kata ya Magoma ambako kumekuwepo na tatizo la maji kwa muda mrefu.
Mkuu wa wilaya ya Korogwe Mrisho Gambo, aliyeongozana na Wakurugenzi wa mji Lewis kalinjuna wa Korogwe Vijijini Lucas Mweri wakati wakimuonesdha eneo litakalochimbwa kisima katika kijiji cha Kwasemangube, alisema walimfuata Sabodo kuomba msaada wa visima kutatua kero ya maji katika maeneo ya wilaya hiyo.
"Tulimfuata sabodo nikiwa na Mbunge wa Korogwe Vijijini, Mbunge wa viti Maalumu mkoa wa Tanga Mary Chatanda ambaye alimuomba visima hivyo ili kusaidia katika jimbo la Korogwe mjini kama unavyojua mama Chatanda, anaishi Korogwe mjini," alisema Gambo.
Mkuu wa wilaya ya Korogwe Mrisho Gambo (Kushoto) akiwa na Kada wa CCM Mustapha Jaffer Sabodo wakati wakizungumza kuhusu ufadhili wa visima katika wilaya ya Korogwe.