Ili kuondoa mkanganyiko ambao umeanza kujitokeza, Wizara inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu tamko lililotolewa na Mhe. Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii.
Aidha, kama ilivyoelezwa katika taarifa mbalimbali za umma zilizokwisha kutolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na TFDA kuhusiana na suala hili, bado inasisitizwa kwamba kampuni ya TPI Ltd iliiuzia Bohari ya Dawa (MSD) dawa bandia aina ya TT-VIR 30 toleo Na. 0C.01.85, kwa mujibu wa nyaraka zilizopo.
Tunapenda kusisitiza kwamba, Mhe. Waziri katika hotuba yake hakukanusha kuwa kampuni ya TPI Ltd iliiuzia MSD dawa bandia bali alieleza kwamba uchunguzi wa awali katika kiwanda cha kampuni hiyo haukuonesha dawa hiyo ilizalishwa na TPI Ltd bali vifungashio ni vya TPI Ltd na nyaraka zinaonesha TPI Ltd kuiuzia MSD dawa hizo bandia.
Aidha, alieleza kuwa vyombo vya usalama bado vinaendelea kulichunguza suala hilo ili kubaini chanzo na wahusika wakuu wa dawa hizo bandia.
Kwa kuzingatia unyeti wa suala hili, Wizara inatoa wito kwa vyombo vya habari kusubiri hatma ya uchunguzi unaofanywa na vyombo vya usalama na kuepuka kutoa taarifa ambazo zinaweza kupotosha umma na jitihada kubwa za Serikali katika kupambana na dawa bandia nchini.
Imetolewa na:
N. Mwamwaja
MSEMAJI WA WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
16 Mei, 2013